×

Lissu Aibua Mapungufu Katika Kesi ya Uhaini, Amtaja ACP Bagyemu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameiambia Mahakama kuwa kesi ya uhaini inayomkabili ina mapungufu kadhaa, akidai kuwa mchakato wa kuanzisha upelelezi wa kesi hiyo ulifanywa na mtu mmoja au watu wachache bila kuwashirikisha baadhi ya mamlaka husika.

Lissu ametoa hoja hizo leo, Jumatatu, Septemba 28, 2026, wakati akiendelea kuwasilisha hoja zake za mwisho mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Katika hoja zake, Lissu amemtaja Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George Bagyemu, anayehudumu kama Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, akidai kuwa ndiye aliyeamua kwamba maneno yaliyokuwa kwenye video yanaunda kosa la uhaini.

Lissu amesema kwa mujibu wa rekodi ya mahakama katika ukurasa wa 145 na 146, tukio hilo lilihusisha hatua zilizochukuliwa Aprili 8, 2025, siku nne baada ya video hiyo kuonekana.

Amedai kuwa baada ya Bagyemu kuipata video hiyo, alifungua faili la uchunguzi wa uhaini bila kuwashirikisha baadhi ya wakuu wake wa kazi, akiwamo Mkuu wa Polisi Kanda Maalum (ZPC) na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Kwa mujibu wa Lissu, Bagyemu aliwafahamisha viongozi hao baada ya faili hilo kufunguliwa.

Lissu pia amedai kuwa Bagyemu hakutafuta ushauri wa kisheria kabla au baada ya kufungua faili hilo. Akirejea ukurasa wa 159 wa rekodi ya ushahidi, amesema suala hilo lilithibitishwa katika ushahidi wa Bagyemu.

Aidha, Lissu amesema hata Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakujulishwa kuhusu suala hilo wakati huo.

Ameongeza kuwa licha ya Bagyemu kuwafahamisha baadhi ya viongozi kuhusu hatua alizochukua, hakuna hata mmoja kati yao aliyefika mahakamani kutoa ushahidi kuhusu suala hilo.

Lissu pia amedai kuwa Bagyemu hakuhusisha wala kutoa taarifa kwa mamlaka nyingine za uchunguzi au taasisi nyingine za Serikali kuhusu hatua hizo.

Katika hatua hiyo ya hoja zake za mwisho, Lissu amesisitiza kuwa jukumu la kuthibitisha mashtaka linabaki upande wa mashtaka, akidai kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani haujafikia kiwango cha uthibitisho kinachotakiwa kisheria.

Leave a Comment