
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi ametoa wiki mbili kwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Fedha na Kilimo kuandaa mpango wa mafunzo kwa Vitendo ambao utaanza kuchukua walau vijana 10,000 kupata uzoefu katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Sekta binafsi ili kuandaa vijana watakaokuwa na uzoefu wa kujiajiri na kuajiriwa kama sehemu muhimu ya kutekeleza nguzo ya pili ya Dira ya Taifa 2050 na kusaidia maendeleo ya Nchi.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma, kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Amewataka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma kubadili namna taasisi hizo zinavyofanya kazi na kuwa injini ya mageuzi ya uchumi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akielekeza kuanzishwa kwa mkakati huo utakaowapatia angalau wahitimu 10,000 nafasi za mafunzo kwa vitendo na kuwapatia fedha za kujikimu katika mashirika ya umma na wengine wasiopungua 20,000 katika sekta binafsi.
“ Kila mwaka kwa takribani vijana 62,570 wanahitimu elimu ya juu na hii ni takwimu ya mwaka Jana 2025 toka TCU, idadi hiyo haihusishi wale wanaomaliza VETA na Vyuo vya Kati.

Ukiangalia TAESA takwimu zao zinaonesha vijana 3,200 pekee walikuwa wamepitia programu za mafunzo internship, idadi hii ni ndogo sana kwa kulinganishwa na wahitimu 62,570 kutoka vyuo mbalimbali nchini.
Mlitazame hili kama uwekezaji wa kimkakati katika nguvu kazi ya Taifa kwa kubana matumizi ya kawaida, na hapa mtakuwa mmetekeza kwa Vitendo nguzo ya pili ya Dira 2050” alisisitiza
Mhe. Ndejembi, amesema dhamana ya Watendaji, Wakuu wa Mashirika na Wenyeviti wa Bodi ni kubwa, na hivyo wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ustadi na umakini mkubwa na kwa wakati sahihi katika kujenga uchumi, kuibua fursa mpya na kuinua maisha ya watanzania.