×

Urusi Yashambulia Ukraine kwa Drones, Watu Wawili Wauawa Sokoni

KYIV, Ukraine – Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) yanayodaiwa kufanywa na Urusi yamesababisha vifo vya watu wawili katika soko lililopo nje kidogo ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, huku watu wengine watatu wakiripotiwa kuuawa katika mashambulizi tofauti katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine, shambulio hilo lilitokea Jumapili, Septemba 27, 2026, katika eneo la Sofiiska Borshchahivka, upande wa magharibi wa Kyiv. Waendesha mashtaka walisema watu wawili waliuawa na takribani wengine 10 kujeruhiwa.

Picha zilizosambazwa baada ya tukio zilionyesha magari na maeneo mbalimbali ya soko yakiwa yamewaka moto, huku mabaki ya vitu vilivyoharibiwa yakionekana kutapakaa eneo la tukio.

Kyiv Yashambuliwa

Katika mji wa Kyiv wenyewe, Meya Vitali Klitschko alisema watu tisa walijeruhiwa, akiwemo mtoto mmoja. Watu sita kati ya waliojeruhiwa walikuwa wakipatiwa matibabu hospitalini.

Klitschko pia alisema drone iligonga jengo refu la makazi katika eneo la mashariki mwa jiji na kusababisha moto, huku mtu mmoja akijeruhiwa.

Baadaye, aliripoti kuwa drone nyingine iligonga jengo lingine refu katika eneo la katikati ya jiji, ambapo huduma za dharura zilifika kufanya tathmini ya hali na kubaini iwapo kulikuwa na majeruhi zaidi.

Maeneo yaliyo karibu na shule ya chekechea na uwanja wa michezo pia yaliripotiwa kushambuliwa.

Vifo Vyaripotiwa Sumy na Kharkiv

Katika mji wa Sumy, kaskazini mwa Ukraine, mabomu matatu ya aina ya glide bombs yaliripotiwa kulipuka karibu na kituo cha kusaidia familia, na kusababisha vifo vya watu wawili, kwa mujibu wa Gavana wa Mkoa wa Sumy, Oleh Hryhorov.

Nchini Kharkiv, mji mkubwa wa pili wa Ukraine uliopo kaskazini-mashariki, waendesha mashtaka walisema drone iligonga gari na kumuua dereva.

Mashambulizi hayo yamekuja katika kipindi ambacho Urusi imeongeza matumizi ya mashambulizi ya anga dhidi ya miji mbalimbali ya Ukraine. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alisema Urusi ilirusha drones 277 za aina mbalimbali tangu Jumamosi, zikiwemo 155 za injini za ndege (jet-powered drones).

Zelenskiy amelaani mashambulizi hayo, akisema kulengwa kwa maeneo ya kiraia ni “ugaidi” na kwamba, kwa mtazamo wake, mashambulizi hayo hayana malengo ya kijeshi.

Miundombinu ya Mawasiliano Yalengwa

Mbali na maeneo ya makazi, miundombinu ya mawasiliano na vituo vya kuhifadhi data pia iliripotiwa kuathiriwa.

Kampuni kubwa zaidi ya huduma za simu nchini Ukraine iliiambia Interfax Ukraine kuwa makao yake makuu yaligongwa katika mashambulizi yanayoendelea dhidi ya vituo vya data na miundombinu ya mawasiliano. Hakuna vifo vilivyoripotiwa katika tukio hilo.

Kwa upande mwingine, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema vikosi vyake vilishambulia vituo viwili vya data jijini Kyiv, kituo cha usafirishaji bidhaa mjini Odesa pamoja na meli mbili za mizigo zilizokuwa zikielekea Odesa.

Mashambulizi hayo yanaendelea huku vita kati ya Urusi na Ukraine vikiingia katika kipindi kingine cha mapigano makali, huku miji na miundombinu ya kiraia ikiendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayoripotiwa kuathiriwa.

Leave a Comment