
KINSHASA, DR Congo – Watu 17 wamefariki dunia baada ya ndege aina ya LET 410 UVP kuanguka na kushika moto karibu na mji wa Kenge, makao makuu ya jimbo la Kwango nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ajali hiyo ilitokea Ijumaa mchana wakati ndege hiyo, iliyokuwa ikiendeshwa na kampuni ya TRACEP Congo Aviation, ikiwa katika safari kutoka Kikwit kuelekea Kinshasa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Uchukuzi, ndege hiyo ilipata hitilafu ya kiufundi na ndipo ikaelekezwa Kenge katika jaribio la kutua kwa dharura. Hata hivyo, mamlaka za eneo hilo zilisema hakukuwa na uwanja wa ndege unaofanya kazi ambao ungeweza kupokea ndege hiyo.

Ndege hiyo ilianguka katika eneo la makazi kabla ya kulipuka na kushika moto. Watu wote 17 waliokuwa ndani yake, wakiwemo abiria 13 na wahudumu wanne, walifariki dunia.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni maafisa wawili waandamizi wa mahakama ya kijeshi ya DRC, Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi Tiende, aliyekuwa Rais wa Mahakama Kuu ya Kijeshi, na Luteni Jenerali Lucien-René Likulia Bakumi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kijeshi wa FARDC.
Awali, taarifa za mamlaka zilitaja vifo vya watu 13, kabla ya idadi hiyo kufikia 17 baada ya shughuli za uokoaji kukamilika.
Serikali Yasitisha Shughuli za TRACEP
Baada ya ajali hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchukuzi, Jean-Pierre Bemba, aliamuru kusimamishwa mara moja kwa Cheti cha Uendeshaji wa Ndege (Air Operator Certificate) cha TRACEP Congo Aviation.
Hatua hiyo imesababisha kusitishwa kwa shughuli za shirika hilo nchini hadi uchunguzi wa ajali hiyo utakapokamilika.
Wachunguzi kutoka mamlaka ya uchunguzi wa ajali za anga nchini humo wamepelekwa katika eneo la tukio ili kubaini chanzo cha ajali na mazingira yaliyopelekea ndege hiyo kuanguka.
Wizara ya Mawasiliano pia imesema Waziri wa Sheria ameagiza uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo ufanyike kwa mujibu wa sheria za nchi.

Tshisekedi Atuma Rambirambi
Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliofariki, huku Serikali ikieleza mshikamano wake na familia hizo, mfumo wa mahakama na wanajeshi walioathiriwa na msiba huo.
Kutokana na ukubwa wa janga hilo, Serikali ya DRC imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
Rais Tshisekedi pia ameagiza bendera ya taifa kupeperushwa nusu mlingoti kuanzia Jumatatu, Septemba 28, hadi siku ya mazishi ya waathiriwa.
Serikali imewataka wananchi kuwa na utulivu, heshima na mshikamano na familia zilizopoteza wapendwa wao.
Aidha, mamlaka zimewaomba wananchi kuepuka kusambaza picha za waathiriwa au taarifa zinazoweza kudhalilisha heshima yao na kuongeza maumivu kwa familia zao.
DR Congo itaendelea na kipindi hicho cha maombolezo ya kitaifa huku uchunguzi wa chanzo cha ajali ukiendelea.