
DAR ES SALAAM: Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ameagiza kusitishwa kwa mfumo wa pointi kwenye leseni za madereva, akisema mfumo huo ulikuwa bado haujaanza kutekelezwa rasmi na ulikuwa katika hatua ya majaribio.
Katambi ametoa agizo hilo leo, Septemba 29, 2026, katika Stendi ya Kimataifa ya Magufuli jijini Dar es Salaam, wakati alipokutana na madereva kufuatia mgomo ulioanza asubuhi ya leo.
Waziri huyo amesema suala la mfumo wa pointi litasitishwa na kufanyiwa tathmini ya kina kwa kuwashirikisha madereva pamoja na viongozi wao.
“Kwa hiyo mpaka sasa ninavyozungumza kwenye jambo hili la pointi, maagizo na maelekezo yangu na uamuzi wangu ni huu, jambo hili lisitishwe na tathmini ya kina itafanyika kwa kuwashirikisha madereva hawa wote kupitia viongozi wao, kuanzia viongozi wa wamiliki,” amesema Katambi.
Ameongeza kuwa viongozi wa madereva na wadau wengine tayari wamekutana Dodoma kwa ajili ya kujadili changamoto zinazohusiana na mfumo huo na kutoa maoni yao.
Mfumo huo unatokana na Tangazo la Serikali Na. 420 (G.N. No. 420), ambapo kila leseni ya udereva ina jumla ya pointi 15 zinazoweza kupunguzwa kulingana na aina na uzito wa kosa la usalama barabarani linalofanywa na dereva.
Agizo hilo limetolewa wakati madereva wa mabasi katika maeneo mbalimbali nchini wakiendelea na mgomo wakipinga, miongoni mwa mambo mengine, mfumo wa pointi, faini na hatua zinazochukuliwa dhidi yao kwa makosa ya usalama barabarani.
Katambi amesema maoni ya madereva yatatumika katika mchakato wa kufanya tathmini ya mfumo huo.