
KYIV: Mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka Urusi yameua watu wanne katika mji wa Kyiv na maeneo ya jirani, huku miundombinu ya nishati ikiharibiwa na mji huo kufunikwa na moshi.
Kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine, wanawake wawili na mtoto mwenye umri wa miaka 14 waliuawa katika mashambulizi ya usiku yaliyolenga Kyiv na mji mmoja uliopo kaskazini mwa mji huo. Mtu mwingine aliuawa katika shambulio dhidi ya ghala moja jijini Kyiv.

Jeshi la Anga la Ukraine limesema Urusi ilitumia makombora ya balistiki na ya kuzuia meli pamoja na ndege zisizo na rubani 188. Ukraine inadai kuwa ilifanikiwa kuzuia makombora matano na ndege hizo zisizo na rubani 155.
Mashambulizi hayo pia yamelenga miundombinu ya nishati katika eneo la Kyiv, wakati Ukraine ikijiandaa kwa msimu mwingine wa baridi. Kampuni ya nishati ya DTEK imesema wafanyakazi wake wamefanikiwa kurejesha huduma ya umeme kwa kaya 8,000, ingawa haikutoa taarifa kamili kuhusu kiwango cha uharibifu.

Urusi imethibitisha kufanya mashambulizi hayo makubwa ya usiku, ikisema imelenga kituo cha data kinachosaidia majeshi ya Ukraine, mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme katika eneo la Kyiv, kituo cha viwanda katika eneo la Odesa na miundombinu ya bandari ya Izmail.
Huko Kyiv, moshi mzito ulitanda katika maeneo mbalimbali kufuatia mashambulizi hayo, huku huduma za dharura zikiwataka wakazi kufunga madirisha ili kujilinda dhidi ya moshi.
Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko, amesema mabaki ya kifaa kilichotumika katika shambulio yalipatikana katika eneo la ubalozi wa nchi ya Magharibi katikati ya jiji, ingawa hakutaja ubalozi huo ni wa nchi gani.

Mashambulizi hayo pia yameleta taharuki katika nchi jirani. Moldova imesema ndege isiyo na rubani ilivuka anga lake na kulipuka karibu na kijiji cha Hirbovet, huku Romania na Poland zikirusha ndege za kijeshi kufuatilia hali hiyo.
Poland pia ilisimamisha kwa muda safari za ndege katika viwanja vya Lublin na Rzeszow.
Wakati huo huo, Ukraine imeendelea kufanya mashambulizi ndani ya Urusi, yakilenga miongoni mwa mengine mitambo ya kusafisha mafuta na maeneo yanayohusishwa na shughuli za kiuchumi za Moscow.
Maafisa wa Urusi wamesema mtu mmoja aliuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika eneo la Bryansk, linalopakana na Ukraine. Mashambulizi mengine ya Ukraine katika eneo la Samara, linalozalisha mafuta, yaliripotiwa kusababisha uharibifu katika baadhi ya nyumba.