
BARIADI: Stendi ya malori iliyojengwa kwa zaidi ya Sh2.8 bilioni katika Mji wa Bariadi, Simiyu, imegeuka kuwa mradi usiotumika ipasavyo, huku wafanyabiashara, madereva na mawakala wa mizigo wakieleza kuwa umbali na ukosefu wa miundombinu muhimu ni miongoni mwa sababu zinazowafanya kuikwepa.
Stendi hiyo iliyobuniwa mwaka 2019 na Halmashauri ya Mji wa Bariadi ililenga kuhudumia malori makubwa ya mizigo yanayoingia na kutoka mjini, kupunguza msongamano wa magari na kuondoa utaratibu wa kupakia na kushusha mizigo katikati ya mji.

Ujenzi wake ulikamilika mwaka 2020 kwa gharama ya zaidi ya Sh2.8 bilioni, lakini takribani miaka sita baadaye, matumizi yake yameendelea kuwa madogo.
Uchunguzi umebaini kuwa ni malori kati ya matano na 10 pekee kwa mwezi yanayotumia stendi hiyo, huku takribani malori 150 kwa mwezi yakitajwa kuendelea kushusha na kupakia mizigo katika maeneo yasiyo rasmi katikati ya mji.
Madereva wanaokwepa stendi hiyo hutozwa faini ya Sh100,000 na Halmashauri, lakini hatua hiyo haijaonekana kuzuia ongezeko la malori yanayoendelea kutumia maeneo yasiyo rasmi.

CAG: Utafiti Haukuwa wa Kutosha
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2025/26 imeibua hoja kuhusu utekelezaji wa mradi huo, ikieleza kuwa utafiti wa kutosha haukufanyika kabla ya kuanzishwa kwa mradi.
Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Simiyu, Fortunatus Donge, amesema Halmashauri ilipaswa kufanya utafiti wa kina kubaini kama mradi huo ungekuwa na manufaa kwa Serikali na wananchi.
“Katika ukaguzi tulichokibaini ni kuwa mradi haukufanyiwa utafiti wa kutosha, mradi umetumia fedha nyingi za umma, lakini hautumiki, malori hayataki kupaki,” amesema Donge.
Ameeleza kuwa kutotumika kwa stendi hiyo ni changamoto katika matumizi ya fedha za umma, huku akishauri Halmashauri kufanya tathmini na kuangalia uwezekano wa kubadilisha matumizi ya eneo hilo.
TAKUKURU Yabaini Wadau Hawakushirikishwa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nayo imebaini changamoto katika utekelezaji wa mradi huo.
Katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha 2023 hadi 2026, TAKUKURU Mkoa wa Simiyu ilibaini kuwa baadhi ya miradi ilitekelezwa bila ushirikishwaji wa kutosha wa wadau.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Simiyu, Aron Misanga, amesema stendi ya malori ni miongoni mwa miradi ambayo wadau hawakushirikishwa kikamilifu.
“Moja ya miradi ambao tulibaini wadau hawakushirikishwa ni stendi hiyo ya malori, tangu umekamilika ni muda mrefu, lakini haitumiki. Wenye magari wamegoma kutumia stendi hiyo,” amesema Misanga.
Umbali Wawalazimisha Wafanyabiashara Kuikwepa
Kwa wafanyabiashara wa Bariadi, umbali wa stendi hiyo ni moja ya sababu kubwa inayowafanya waendelee kushusha mizigo katikati ya mji.
Stendi hiyo ipo takribani kilomita saba kutoka katikati ya Bariadi, jambo linalowalazimisha wafanyabiashara kutumia gharama za ziada kusafirisha mizigo kutoka stendi hadi madukani.
Neema Shija, mfanyabiashara wa nafaka, amesema gharama hizo ni mzigo kwa wafanyabiashara wenye mitaji midogo.
“Ukiishushia humo ndani, unatakiwa kutafuta gari ndogo au bajaji kuleta mzigo hadi mjini na gharama zake ni kubwa,” amesema.
Jumanne Singibala, mfanyabiashara wa mbao, amesema umbali huo unawalazimisha kufanya safari nyingi za kusafirisha mizigo.
Amesema gharama ya gari ndogo kusafirisha mzigo kutoka stendi hadi mjini ni kati ya Sh40,000 na Sh50,000 kwa safari moja.
Mfanyabiashara mwingine, Manase Shingile, amesema amewahi kutumia stendi hiyo lakini gharama za kusafirisha mzigo kutoka eneo hilo hadi mjini zilikuwa kubwa.
Usalama wa Mizigo Nao Watajwa
Mbali na umbali, wafanyabiashara wameeleza ukosefu wa sehemu maalumu za kuhifadhi mizigo kuwa changamoto nyingine.
Henry Shabani amesema hali huwa mbaya zaidi wakati wa mvua kwa sababu hakuna ghala au eneo salama la kuhifadhi mizigo.
“Wakati stendi inaanza kufanya kazi, tulianza kushushia huko, lakini tulipata shida sana mvua zilipoanza kunyesha. Mizigo ya wafanyabiashara ilinyeshewa mvua na tukapata hasara kubwa,” amesema.
Mawakala wa mizigo nao wameeleza kuwa changamoto hizo zimefanya wafanyabiashara kutafuta maeneo mengine ya kushushia mizigo.
Jumanne Kiyumbi, mmoja wa mawakala, amesema hakuna mfanyabiashara aliye tayari kuongeza gharama kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo kutoka stendi hiyo hadi mjini.
Stendi Bubu Yaibuka
Kwa mujibu wa Julius Mlangila, wakala wa mizigo, kutotumika kwa stendi rasmi kumesababisha kuibuka kwa maeneo yasiyo rasmi ya kushushia mizigo.
Amesema baadhi ya malori yanashusha mizigo katika maeneo hayo licha ya kutozwa Sh100,000 na Halmashauri.
“Kila gari linalofika kushusha mzigo kwenye eneo letu jipya, Halmashauri wanachukua ushuru (faini), kila gari linalipia Sh100,000 na wafanyabiashara wapo tayari kulipa hicho kiasi na siyo kushushia kwenye ile stendi,” amesema Mlangila.
Madereva Walalamikia Huduma
Madereva nao wamesema eneo hilo halina huduma muhimu zinazoweza kuwafanya wabaki hapo wakati wa kusubiri kupakia au kushusha mizigo.
Jafari Mohamed, dereva wa lori, amesema eneo hilo halina nyumba za kulala wageni wala migahawa ya kutosha.
“Hili eneo ni kama porini, hakuna nyumba ya kulala wageni au mgahawa wa chakula. Dereva unafika hapa umechoka, inakulazimu upaki gari humu ndani, kisha uchukue bodaboda kwa gharama ya Sh5,000 ndiyo upelekwe mjini,” amesema.
Halmashauri Yakiri Changamoto
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Idd Ndabhona, amekiri kuwa stendi hiyo haitumiki kwa kiwango kilichokusudiwa, lakini amesema uongozi unaendelea kufanyia kazi ushauri wa CAG na TAKUKURU.
Ndabhona amesema eneo hilo lilichaguliwa kutokana na matarajio ya ukuaji wa Mji wa Bariadi na nia ya kupunguza msongamano katikati ya mji.
“Kweli ni mbali, lakini huo ulikuwa ushauri wa kitaalamu ijengwe kule kutokana na mji kukua kila wakati. Tuliwaza mbele zaidi ili kupunguza msongamano mjini,” amesema.
Amesema Halmashauri imebaini changamoto zinazohusu usalama wa mizigo na matumizi ya stendi na inaendelea kufanya tathmini ya mradi huo.
“Watalaamu watakaa na kupitia changamoto zote, ufanisi wa mradi kama ambavyo tumeshauriwa, kisha tutakuja na jibu kama tuibadilishie matumizi au tufanye jambo gani,” amesema.
Ushauri wa Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema uchunguzi alioufanya awali ulibaini kuwa utafiti wa kutosha haukufanyika kabla ya mradi kutekelezwa.
Macha amesema sababu zilizotolewa na wafanyabiashara kuhusu umbali na usalama wa mizigo zina msingi.
Ameshauri Halmashauri kufanya tathmini upya ya mradi huo na kuangalia matumizi mengine yanayoweza kulifanya eneo hilo liwe na tija.
“Mimi nadhani ushauri wa CAG ufanyiwe kazi, mradi umekuwa hasara kwa Halmashauri. Fanyeni tathmini upya kuangalia ni mradi gani mwingine unaweza kutekelezwa pale na ukaleta ufanisi kwenye Halmashauri,” amesema Macha.
Kwa sasa, stendi hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya kupata watumiaji, huku malori yakiendelea kushusha na kupakia mizigo katikati ya Bariadi licha ya kuwepo kwa miundombinu iliyogharimu mabilioni ya fedha za umma.
Stori na Derick Nilton | GPL -Bariadi