×

Rick Ross Akamatwa Miami Kwa Mashtaka ya Unyanyasaji wa Mwili

Msanii wa muziki wa Marekani Rick Ross, ambaye jina lake halisi ni William Roberts II, amekamatwa jijini Miami, Florida, kwa mashtaka mawili ya kumpiga na kumshambulia aliyekuwa mpenzi wake, Jazzma Kendrick.

Ross alijisalimisha mwenyewe kwa polisi Alhamisi, Oktoba 1, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi zilizonukuliwa, Kendrick alidai kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 28 katika nyumba ambayo wawili hao walikuwa wakiishi.

Inadaiwa kuwa Kendrick alikuwa amelala wakati Ross alipomwamsha na kuanza kumuuliza kuhusu picha aliyokuwa ametagiwa kwenye mitandao ya kijamii. Mazungumzo hayo yalidaiwa kugeuka kuwa ugomvi, ambapo Kendrick alisema Ross alimpiga kofi usoni.

Aliendelea kudai kuwa Ross alimpiga mara kadhaa kifuani, kabla ya kumkaba shingoni kiasi cha kumfanya ashindwe kupumua. Pia alidai kuwa Ross alimvuta kwa nywele zake na kumsukumia ukutani.

Kendrick aliripotiwa kuwasilisha kwa polisi picha ambazo anadai zinaonyesha majeraha aliyoyapata.

Ross, ambaye bado yuko kwenye mchakato wa kesi, amekana mashtaka hayo na amedai hana hatia. Mawakili wake, Steve Sadow na Bradley Horenstein, wamesema mteja wao ameshtakiwa kwa makosa na kwamba sababu za aliyekuwa mpenzi wake kutoa madai hayo hazijaeleweka.

Mawakili hao pia wameeleza kuwa madai hayo yaliwasilishwa kwa polisi takribani mwezi mmoja baada ya tukio linalodaiwa kutokea, huku wakiiomba jamii kutohukumu kabla ya mchakato wa kisheria kukamilika.

Rick Ross amewekewa dhamana ya jumla ya takribani TSh milioni 15.6, ambapo TSh milioni 13 ni kwa shtaka la kumkaba na TSh milioni 2.6 kwa shtaka la kumpiga.

Anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka tarehe 22 Oktoba 2026.

Kwa sasa, madai dhidi ya Rick Ross bado hayajathibitishwa mahakamani, na kesi inaendelea kupitia mchakato wa kisheria.

Leave a Comment