×

Elimu ya fedha kuimarisha uwezo wa wahitimu kufanya maamuzi sahihi

DAR ES SALAAM: Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema ujumuishaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi utawajengea wanafunzi na wahitimu uwezo wa kusimamia fedha na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.

Amesema elimu hiyo pia itawawezesha vijana kutumia fursa za kiuchumi kwa tija na kukabiliana na changamoto za kifedha wanapoingia katika soko la ajira.

Ameir ameyasema hayo Oktoba 2, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Ujumuishaji wa Elimu ya Fedha katika mitaala.

Amesema kupitia mwongozo huo, wanafunzi watajengewa uelewa kuhusu namna ya kupanga mapato na matumizi, kuweka akiba, kukopa kwa uwajibikaji pamoja na kutambua na kutumia fursa za uwekezaji.

“Nazielekeza taasisi za elimu ya juu, TCU, NACTVET na VETA kusimamia ujumuishaji wa elimu ya fedha katika mitaala na mifumo ya udhibiti wa ubora, huku taasisi za fedha na washirika wa maendeleo wakishirikiana na vyuo kutoa mafunzo kwa vitendo, ushauri wa kitaalamu na programu za ujasiriamali,” amesema.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, mafanikio ya mwongozo huo hayataangaliwa kwa kuishia kwa wanafunzi kupata maarifa pekee, bali kwa uwezo wao wa kuyatumia katika kufanya maamuzi yenye uwajibikaji wa kifedha.

Amesema hatua hiyo inatarajiwa pia kuwasaidia wahitimu kujiajiri, kuajiri wengine na kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemo, amesema mwongozo huo unakamilisha juhudi za Serikali za kuhakikisha elimu ya fedha inakuwa sehemu ya mfumo rasmi wa elimu nchini.

Msemo amesema Benki Kuu itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi nyingine katika kutoa utaalamu, kujenga uwezo wa wahadhiri na kufuatilia utekelezaji wa mwongozo huo.

Amesema ujumuishaji wa elimu ya fedha katika mitaala ni hatua muhimu katika kuwajengea wanafunzi na wahitimu uwezo wa kusimamia fedha zao kwa ufanisi na kujenga ustahimilivu wa kifedha.

Mwongozo huo unalenga kuhakikisha wanafunzi na wahitimu wanakuwa na maarifa na ujuzi wa kifedha unaoweza kuwasaidia katika maisha yao binafsi, shughuli za kiuchumi na hatimaye kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Leave a Comment