
Mlimbwende wa Tanzania katika mashindano ya Miss Grand International 2026, Jihan Mohin Dimack, ameendelea kuonyesha ushindani mkubwa baada ya kuongoza katika hatua ya tatu ya upigaji kura wa kipengele cha Country’s Power of the Year.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyooneshwa kwenye tovuti rasmi ya mashindano hayo, Jihan aliongoza kwa kupata asilimia 32 ya kura, akifuatiwa na Shyare Andrade wa Ecuador aliyepata asilimia 15.
Ignacia Michelson wa Chile alishika nafasi ya tatu kwa asilimia 13, huku Emoura Phạm wa Vietnam akimaliza katika nafasi ya nne kwa asilimia 12.
Matokeo hayo yameiwezesha Tanzania kuingia kwenye Final 4 ya kipengele cha Country’s Power of the Year pamoja na Ecuador, Chile na Vietnam.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi za mashindano hayo, Round 3 ilikuwa na ushindani mkubwa, huku nafasi zikibadilika hadi muda wa mwisho wa upigaji kura kabla ya zoezi hilo kufungwa rasmi.
Mbali na mafanikio hayo, Tanzania pia imeendelea kufanya vizuri katika kipengele cha Miss Popular, ambapo kwa sasa inaongoza kwa kupata asilimia 19 ya kura, ikifuatiwa na Vietnam yenye asilimia 17.
Matokeo hayo yanaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazopata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa mashabiki katika hatua hii ya mashindano.
Baada ya kukamilika kwa Round 3, waandaaji wa Miss Grand International wametangaza kuwa kanuni za Round 4 zitatolewa hivi karibuni, huku mashabiki wakitakiwa kujiandaa kuendelea kuonyesha nguvu ya nchi zao.
Watanzania wanaendelea kuhamasishwa kumuunga mkono Jihan Mohin Dimack katika hatua zinazofuata za mashindano hayo, huku kila kura ikiwa na mchango katika safari yake ya kuiwakilisha Tanzania kwenye Miss Grand International 2026.
🇹🇿 Tanzania imeingia Final 4. Sasa nguvu inaelekezwa kwenye Round 4.
