Mlimbwende wa Tanzania katika mashindano ya Miss Grand International 2026, Jihan Mohin Dimack, amewashukuru Watanzania kwa kumpa sapoti kubwa iliyoiwezesha Tanzania kuingia katika Top 4 ya tuzo ya “Country Powerhouse of the Year”.
Jihan amesema mafanikio hayo si yake binafsi, bali ni matokeo ya mshikamano wa Watanzania waliopiga kura, kushiriki machapisho, kuhamasisha wengine na kuendelea kumpa moyo katika safari yake ya kuiwakilisha Tanzania kimataifa.
Akizungumza baada ya Tanzania kufanikiwa kuingia Top 4, Jihan amesema amejawa na furaha na shukrani, akieleza kuwa kila kura na kila juhudi iliyofanywa na Watanzania imekuwa sehemu muhimu ya safari yake.
“Huenda ni mimi ninayesimama hapa leo, lakini mafanikio haya yana sehemu ya kila mmoja wenu,” amesema Jihan.
Mlimbwende huyo ametoa shukrani zake kwa Watanzania kwa maneno mbalimbali, akiwashukuru kwa kumpokea, kumpenda, kumuamini na kumuunga mkono katika safari yake ya Miss Grand International 2026.
Jihan amesema hatua hiyo imeonyesha nguvu ya umoja wa Watanzania, akisisitiza kuwa kutoka Tanzania hadi kwenye jukwaa la kimataifa, wameweza kuonyesha kwamba mshikamano unaweza kuleta matokeo makubwa.
Kwa upande wake, Jihan ameendelea kuhamasisha Watanzania kuendelea kuwa sehemu ya safari yake huku akitambua mchango wa kila mmoja aliyeshiriki kuhakikisha Tanzania inafika katika hatua hiyo.

