
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeagiza shule zote za msingi na sekondari Tanzania Bara kufungwa Novemba 13, 2026, badala ya Desemba 4, 2026 kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Uamuzi huo umetangazwa kupitia Waraka wa Elimu Na. 3 wa Mwaka 2026 kuhusu mabadiliko ya tarehe ya kufunga shule za awali, msingi na sekondari Tanzania Bara, uliotolewa na Wizara hiyo tarehe 30 Septemba 2026.
Kwa mujibu wa waraka huo, hatua hiyo imechukuliwa kufuatia taarifa za hali ya hewa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa zinazohusishwa na El Niño katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.
Wizara imeeleza kuwa mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko na athari nyingine katika baadhi ya maeneo, hivyo hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama na ustawi wa wanafunzi, walimu pamoja na watumishi wengine wa shule.
Awali, kupitia Waraka wa Elimu Na. 6 wa Mwaka 2025 kuhusu kalenda ya mihula ya masomo kwa mwaka 2026 na Waraka wa Elimu Na. 1 wa Mwaka 2026 kuhusu kalenda ya mihula kwa Kidato cha Tano na Sita kwa mwaka wa masomo 2026/2027, shule zilipangwa kufungwa tarehe 4 Desemba 2026.
Hata hivyo, Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene M. Mtahabwa, ametangaza kuwa shule zote zifungwe tarehe 13 Novemba 2026, ikiwa ni hatua ya tahadhari kutokana na utabiri wa hali ya hewa.
Waraka huo umeelekeza kuwa uamuzi huo unaanza kutumika rasmi kuanzia Oktoba 1, 2026.
Wizara imetoa waraka huo kwa wadau mbalimbali wa elimu, wakiwemo TAMONGSCO, Christian Social Services Commission (CSSC), BAKWATA, Tanzania Association of Private Investors in Education (TAPIE), Baraza la Sunnar Tanzania (BASUTA), TEN/MET, TAWOSCO pamoja na Umoja wa Wazazi wa CCM.
