DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh trilioni 10.65 katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, ikiwa ni asilimia 107.49 ya lengo la Sh trilioni 9.91 lililowekwa kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Kwa mujibu wa taarifa ya utendaji kazi ya robo hiyo, makusanyo hayo yameongezeka kwa asilimia 18.81 ikilinganishwa na Sh trilioni 8.96 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2025/2026.
Katika kipindi hicho, TRA pia imekamilisha uchunguzi wa mashauri 130 ya ukwepaji kodi yenye thamani ya Sh bilioni 331.15, huku ikifanikiwa kukusanya Sh bilioni 44.74.
Mamlaka hiyo imesema itaendelea kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya mianya inayosababisha Serikali kupoteza mapato, ikiwemo vitendo vya ukwepaji kodi, biashara za magendo na ukiukaji wa maadili kazini.
Katika udhibiti wa mipaka, TRA imefanya operesheni 1,185 za kufuatilia uingizaji wa mizigo kwa njia zisizo rasmi. Operesheni hizo zilisababisha kukamatwa kwa bidhaa za magendo zenye thamani ya Sh bilioni 12.72 na kuokoa kodi ya Sh bilioni 5.34.
Aidha, ukaguzi wa mizigo na magari 47,773 yanayohusika na usafirishaji wa mizigo umebaini makosa 197 ya udanganyifu, hatua iliyoiwezesha TRA kukusanya Sh bilioni 79.68.
Akieleza hatua zinazochukuliwa kuimarisha nidhamu na uwajibikaji ndani ya taasisi hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, amesema watumishi 1,028 wamepatiwa mafunzo kwa lengo la kuboresha ujuzi katika usimamizi wa sheria za kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
“TRA imewapatia mafunzo watumishi 1,028 ili kuboresha ujuzi wao katika usimamizi wa sheria za kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa TRA imeimarisha pia maadili ya watumishi kwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi tisa waliobainika kuwa na changamoto mbalimbali za kimaadili katika kipindi hicho.
Katika eneo la migogoro ya kodi, TRA imesema imetatua mashauri 10 yaliyokuwa mahakamani yenye thamani ya Sh bilioni 7.78.
Kwa mujibu wa Mamlaka hiyo, hatua hiyo inalenga kuongeza usawa katika utekelezaji wa sheria za kodi na kuweka mazingira salama zaidi kwa biashara na uwekezaji nchini.
TRA imesema itaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato, udhibiti wa magendo na ukwepaji kodi pamoja na uwajibikaji wa watumishi ili kuhakikisha Serikali inapata mapato yanayostahili.

