×

Kyle Simbwa Aibuka Msanii Mpya wa Apple Music Afrika Mashariki

KAMPUNI kubwa ya muziki duniani, Apple Music, imemtangaza mwanamuziki kutoka Uganda, Kyle Simbwa, kuwa msanii mpya wa programu yake ya Up Next Afrika Mashariki, hatua inayompa nafasi ya kuonekana zaidi katika jukwaa la muziki la kimataifa.

Simbwa anatokea Kasangati, mji mdogo uliopo nje ya Kampala, Uganda, na amekuwa akijenga muziki wake kwa kuchota msukumo kutoka katika aina mbalimbali za muziki, ikiwemo R&B na Soul za miaka ya 1990, Synth-pop ya miaka ya 1980, A.O.R., muziki wa Disney TV, Afrobeats na Hip-Hop.

Mchanganyiko huo wa vyanzo tofauti vya muziki umemsaidia kujenga sauti yake inayochanganya Afrobeat na Alté, huku akijikita katika kutengeneza mtindo unaomtambulisha kama msanii wa kizazi kipya cha Afrika Mashariki.

Akizungumza na Apple Music kuhusu kuchaguliwa kwake kwenye mpango wa Up Next Afrika Mashariki, Simbwa amesema hatua hiyo ina maana kubwa kwake na anaamini inawakilisha kizazi kipya cha wasanii wa Afrika wanaojenga utambulisho wao kupitia muziki.

“Kuchaguliwa kwenye Up Next Afrika Mashariki na Apple Music kunamaanisha mengi kwangu kwa sababu mimi ni sehemu ya kizazi cha wasanii wa Kiafrika kinachojenga kitu ambacho ni chetu kipekee,” amesema Simbwa.

Ameongeza kuwa anatamani muziki wake uwafikie watu wengi zaidi na kuwafanya waelewe chimbuko lake la kisanii.

“Nataka watu wasikie muziki wangu, wahisi ninakotoka, na waone jinsi unavyoweza kusafiri mbali,” amesema.

Akizungumzia mipango yake ya mwaka 2026, Simbwa amesema analenga kuongeza kasi katika kazi zake za muziki na kuendelea kuiwakilisha Uganda pamoja na Afrika Mashariki katika majukwaa makubwa.

“2026 ni wa kuchukua kila kitu nilichokuwa nakijenga na kukisukuma mbele zaidi. Rekodi zaidi, kufuatilia mawazo makubwa zaidi, na kuendelea kuiwakilisha Uganda na Afrika Mashariki kwenye jukwaa kubwa zaidi,” amesema.

Simbwa pia anahusika kwa karibu katika hatua mbalimbali za utengenezaji wa muziki wake, kuanzia uandishi wa nyimbo, utayarishaji, urekodi hadi uchanganyaji.

Ushiriki huo wa moja kwa moja katika mchakato wa ubunifu umempa nafasi ya kujaribu mitindo mbalimbali na kuendelea kukuza sauti yake binafsi.

Baada ya kuachia mradi wake wa kwanza, “Person,” mwaka 2025, Simbwa ameendelea kujenga katalogi yake kupitia nyimbo kama “Mwana Gwe,” “Love Me or Don’t,” na “East African Girl.”

Ukuaji wake katika upande wa maonyesho ya moja kwa moja pia umeendelea kuonekana, ikiwa ni pamoja na kutumbuiza katika Xpressions na Afro Urban, ambako amepata nafasi ya kushirikiana jukwaani na wasanii kama Mike Kayihura na Kohen Jaycee.

Kwa sasa, Simbwa anaanza sura mpya ya safari yake ya muziki kupitia “East African Summer,” EP yenye nyimbo saba inayogusa mada za mapenzi, maisha ya usiku, uhuru, safari na uzoefu wa pamoja unaoendelea kuunda utamaduni mpya wa vijana wa Afrika Mashariki.

Kupitia uteuzi huo wa Apple Music, Simbwa anaingia katika hatua mpya ya safari yake ya muziki huku akilenga kuitambulisha sauti yake na ya Afrika Mashariki kwa hadhira pana zaidi.

Leave a Comment