×

Watatu Wauawa, 36 Kujeruhiwa katika Mashambulizi ya Viwanja vya Ndege Saudi Arabia

RIYADH, Saudi Arabia — Watu watatu wameuawa na wengine 36 kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyolenga viwanja viwili vya ndege nchini Saudi Arabia, mamlaka za usafiri wa anga zimesema.

Miongoni mwa waliouawa ni wanawake wawili, raia wa Morocco na Algeria, ambao walipoteza maisha katika shambulio lililolenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abha, mkoani Asir, kusini mwa Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa mamlaka, watu 28 walijeruhiwa katika shambulio hilo, baadhi yao wakiwa katika hali mbaya. Waliojeruhiwa ni pamoja na raia wa Bangladesh na Ufilipino.

Shambulio jingine lilitokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid mjini Riyadh, ambapo mwanaume mmoja raia wa Sudan aliuawa na watu wengine wanane kujeruhiwa. Miongoni mwa waliojeruhiwa ni raia wawili wa Misri na mmoja wa Pakistan.

Mamlaka zimesema majeruhi wote walipelekwa hospitalini mara moja kwa ajili ya matibabu.

Mashambulizi hayo pia yalisababisha uharibifu katika viwanja hivyo vya ndege, huku mamlaka zikisema zinaendelea kufanya tathmini ya kiwango cha uharibifu.

Tukio hilo linakuja wakati mvutano wa kiusalama kati ya Saudi Arabia na wapiganaji wa Houthi nchini Yemen ukiendelea. Jeshi la Saudi Arabia limesema ulinzi wake wa anga uliidungua kombora la balistiki lililorushwa kuelekea eneo la kaskazini mwa Riyadh.

Baadaye, Meja Jenerali Turki Al-Maliki alisema jukwaa lililotumika kurushia kombora hilo liliharibiwa mjini Sana’a, Yemen, wakati wapiganaji wakijiandaa kwa shambulio dhidi ya Saudi Arabia.

Mamlaka za Saudi Arabia zimesema zitaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha usalama wa abiria na wafanyakazi pamoja na kulinda usalama wa mfumo wa usafiri wa anga nchini humo.

Leave a Comment