×

Stanbic Yafungua Milango ya Mitaji Kukuza Sekta ya Kahawa Tanzania

Benki ya Stanbic Tanzania imeahidi kuimarisha ushirikiano na Serikali pamoja na wadau wa sekta ya kahawa nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mitaji, kupanua biashara na kufungua fursa zaidi za masoko ya ndani na kimataifa.

Ahadi hiyo imetolewa wakati wa Tamasha la Kahawa 2026 lililofanyika kuanzia Oktoba 8 hadi 10 katika viwanja vya Tanganyika Coffee Curing, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, likiwakutanisha wakulima, wachakataji, wafanyabiashara na taasisi za fedha.

Kupitia tamasha hilo, Stanbic ilieleza namna huduma zake za kifedha zinavyoweza kusaidia wadau kukuza shughuli zao katika mnyororo mzima wa thamani wa kahawa, kuanzia uzalishaji hadi uchakataji, usafirishaji na biashara ya kimataifa.

Suluhisho zilizowasilishwa na benki hiyo ni pamoja na mikopo ya biashara, ufadhili wa ununuzi wa magari na vifaa, pamoja na huduma za kifedha zinazorahisisha biashara za kimataifa.

Akizungumza baada ya kupokea cheti cha kutambua ushiriki wa Stanbic katika tamasha hilo, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa benki hiyo, Benifrida Tarimo, alisema taasisi hiyo itaendelea kuweka msisitizo katika kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa sekta ya kahawa.

Tarimo alipokea cheti hicho kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliyekuwa mgeni rasmi katika kilele cha tamasha hilo.

Alisema sekta ya kahawa ina fursa nyingi za kiuchumi, hivyo upatikanaji wa mitaji na huduma sahihi za kifedha ni muhimu katika kuwawezesha wadau kuongeza uzalishaji, kupanua biashara na kunufaika na masoko mbalimbali.

“Sekta ya kahawa ina fursa nyingi, kuanzia uzalishaji na uchakataji hadi usafirishaji na masoko ya kimataifa. Kama benki, dhamira yetu ni kuwawezesha wadau kupata mitaji na huduma za kifedha zinazohitajika ili kukuza biashara zao na kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi,” alisema Tarimo.

Hatua hiyo inakuja wakati sekta ya kahawa nchini ikionesha ukuaji wa uzalishaji, ambapo takwimu za Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) zinaonesha kuwa uzalishaji uliongezeka kutoka tani 50,530 katika msimu wa 2024/25 hadi tani 76,470 katika msimu wa 2025/26.

Ongezeko hilo linaonesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kifedha na kibiashara ili kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Prof. Aurelia Kamuzora, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora na kuongeza thamani ya kahawa inayozalishwa nchini.

Alisema juhudi za pamoja zinaweza kuimarisha ushindani wa kahawa ya Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa, huku zikiongeza manufaa kwa wakulima na washiriki wengine wa mnyororo wa thamani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta ya kahawa.

Mnzava alibainisha kuwa kahawa ina mchango muhimu katika uchumi wa nchi kupitia kuongeza kipato cha wakulima, kutengeneza ajira na kukuza mapato ya taifa.

Alisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu za Serikali, taasisi za fedha, wawekezaji na wadau wengine ili kuhakikisha fursa zinazopatikana katika sekta hiyo zinawanufaisha Watanzania wengi zaidi.

Tamasha la Kahawa 2026 lilitoa nafasi kwa washiriki kubadilishana uzoefu, kujenga mahusiano ya kibiashara na kujadili mikakati ya kuongeza thamani ya kahawa ya Tanzania.

Kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo, Stanbic inalenga kuchangia upatikanaji wa huduma za kifedha zitakazosaidia biashara kukua na kuimarisha nafasi ya kahawa ya Tanzania katika masoko ya ushindani.

Leave a Comment