
Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, ametangazwa kuwa Kiongozi wa kundi jipya la Kijeshi na kisiasa linaloitwa Front Pour la Refondation de la Nation (FRN).
Kundi hilo lilitangazwa Jumatatu, Oktoba 12, 2026, katika mji wa Goma, Mashariki mwa DRC, likisema linalenga kuunganisha nguvu za wanaopinga Serikali ya Kinshasa ili kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Katika taarifa iliyosomwa na Claude Ibalanky, aliyewahi kuwa Mshauri wa Rais Félix Tshisekedi, waanzilishi wa FRN walisema wanakusudia kuikomboa nchi na kukomesha kile wanachokiita utawala wa kimabavu.

Walisema wako tayari kutumia njia mbalimbali, ikiwemo nguvu, kufikia malengo yao.Uamuzi wa kumteua Kabila kuongoza kundi hilo unafuatia hotuba aliyotoa siku tatu zilizopita, ambapo aliishutumu Serikali ya Tshisekedi kwa kukiuka misingi ya utawala wa kikatiba, kusimamia vibaya uchumi na kushindwa kukabiliana na changamoto za usalama.
Pia aliituhumu Serikali kuwakamata bila sababu za msingi wapinzani wa kisiasa na baadhi ya Wanajeshi.
Hadi wakati wa kutolewa kwa taarifa hiyo, serikali ya Kinshasa ilikuwa haijatoa tamko rasmi kuhusu kuanzishwa kwa FRN.
Kabila aliongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi Januari 2019, alipokabidhi madaraka kwa Félix Tshisekedi baada ya uchaguzi uliokuwa na utata.
Kutangazwa kwake kuwa Mkuu wa FRN kunaashiria hatua muhimu katika kujihusisha kwake moja kwa moja na kundi lenye silaha linalopinga serikali ya Kinshasa.
Stori na Elvan Stambuli, Global Digital | GPL