×

Makamu wa Rais Ashiriki Misa ya Kumuombea Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere


SUMBAWANGA, OKTOBA 14, 2026 — Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameshiriki Ibada ya Misa Takatifu ya kumuombea Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika kumbukizi ya miaka 27 tangu kifo chake.
Ibada hiyo imefanyika leo, Oktoba 14, 2026, katika Kanisa Katoliki Parokia ya Epifania, Jimbo Katoliki Sumbawanga, mkoani Rukwa.Misa hiyo imeongozwa na Askofu Mstaafu Damian Kyaruzi wa Jimbo Katoliki Sumbawanga na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba; mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere; Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, pamoja na viongozi mbalimbali, waumini na wananchi.

Ibada hiyo ni sehemu ya kumbukizi ya maisha na urithi wa Mwalimu Nyerere, aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999, na kutambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika kupigania uhuru wa Tanganyika, kujenga misingi ya taifa na kuimarisha umoja na mshikamano wa Watanzania.

Kumbukizi hiyo inatoa fursa kwa Watanzania kuendelea kutafakari misingi ya uongozi, uzalendo, amani na umoja wa kitaifa iliyoachwa na Baba wa Taifa, pamoja na umuhimu wa kuendeleza tunu hizo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Comment