
DODOMA/DAR ES SALAAM: Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amesema jopo la mawakili wanaojitolea kumwakilisha limefungua shauri la kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Dodoma, kupinga uhalali wa shauri la kinidhamu linaloendelea dhidi yake.
Katika taarifa yake kwa mawakili na umma, Mwabukusi amesema shauri hilo linahoji uamuzi wa kumfungulia shauri yeye binafsi, akieleza kuwa masuala yanayohusika yanatokana na azimio la kitaasisi.Amesema shauri hilo linatarajiwa kutajwa mahakamani Oktoba 16, 2026, hatua ambayo ni sehemu ya
jitihada za kisheria zinazofanywa na jopo hilo kupinga mwenendo wa shauri la kinidhamu dhidi yake.
Aidha, Mwabukusi ameeleza kuwa mawakili hao wamekata rufaa kupinga uamuzi wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili uliowanyima fursa ya kuwasilisha majibu ya ziada, yanayojulikana kisheria kama rejoinder, pamoja na muda wa kutosha kujiandaa na kutoa ufafanuzi baada ya wakili wake kujiondoa kwenye shauri hilo.Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rufaa hiyo bado inasubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.
Katika hatua nyingine, Mwabukusi amesema amepokea wito wa kufika katika ofisi za Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam (ZCO), leo asubuhi ya Oktoba 15, 2026.
Amesema ataitikia wito huo akifuatana na jopo la mawakili wanaojitolea kumwakilisha, ambao watamsindikiza katika hatua hiyo.
Akizungumzia Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mwabukusi amesema chombo hicho ni tofauti na TLS na hakiko chini ya chama hicho. Ameongeza kuwa muundo wa kamati hiyo unahusisha watumishi wa Serikali na Mahakama.
Amesisitiza kuwa jopo la mawakili wanaomwakilisha linaendelea kutumia njia za kisheria zilizopo kutafuta haki na kuhakikisha taratibu za sheria pamoja na haki ya kusikilizwa vinazingatiwa.
Mwabukusi amewataka mawakili na wananchi kufuatilia taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya masuala hayo, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu na kuzingatia misingi ya utawala wa sheria.