×

Papa Leo XIV Atoa Ujumbe wa Kwanza Baada ya Upasuaji, Aomba Maombi Yaendelee

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, amewashukuru waumini kwa maombi yao ya kumtakia afya njema, ikiwa ni ujumbe wake wa kwanza tangu kufanyiwa upasuaji wa saratani ya mapafu mjini Roma, Italia.

Katika ujumbe wake kwa waumini walioshiriki kongamano la kuadhimisha miaka 10 tangu kutolewa kwa waraka wa Amoris Laetitia, ulioandikwa na mtangulizi wake, Papa Francis, kuhusu familia na wanandoa, Papa Leo XIV amesema ameguswa na maombi pamoja na mshikamano wao.

“Nawashukuru kwa dhati kwa maombi yenu na kazi mliyofanya kwa pamoja.

Kubadilishana uzoefu na kusikilizana kwa makini ni zawadi kubwa kwa Kanisa zima. Tafadhali endeleeni kuniombea, nami ninawaombea,” alisema Papa Leo XIV.

Kwa mujibu wa taarifa za madaktari waliomhudumia, Papa Leo XIV aligundulika kuwa na saratani ya mapafu aina ya pulmonary adenocarcinoma wakati wa upasuaji uliofanyika mjini Roma, ambapo sehemu ya chini ya pafu lake moja iliondolewa.

Madaktari Luigi Carbone na Stefano Margaritora wamesema hali yake inaendelea kuimarika kama ilivyotarajiwa. Papa huyo pia ameweza kutembea ndani ya chumba chake hospitalini, huku akishiriki ibada ya Misa pamoja na mapadre wengine katika eneo maalumu lililoandaliwa hospitalini humo.

Papa Leo XIV alikuwa ametangaza mpango wa kufanyiwa upasuaji huo katika hotuba yake kwa waumini waliokuwa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, akieleza kuwa uvimbe uliokuwa kwenye pafu lake uligundulika katika hatua za awali.

Kutokana na matibabu hayo, Papa Leo XIV amesitisha shughuli zake zote za hadhara hadi Oktoba 20, 2026. Hata hivyo, anatarajiwa kufanya ziara ya muda mrefu katika Amerika Kusini mwezi Novemba, iwapo hali yake ya kiafya itaruhusu.

Leave a Comment