×

Mwigulu Aagiza Wananchi wa Miji Midogo Kuunganishiwa Umeme kwa Shilingi 27,000

BAGAMOYO, PWANI — Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kuwaunganishia umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000 wananchi wa maeneo yaliyopandishwa hadhi kuwa miji midogo lakini bado yana mazingira na hali za maisha zinazofanana na vijijini.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 16, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, katika ziara yake ya kikazi ya siku moja.

Amesema kupandishwa kwa hadhi ya eneo kutoka kijiji hadi mji mdogo hakumaanishi moja kwa moja kuwa wananchi wake wameongezeka kipato au uwezo wa kumudu gharama kubwa za huduma za kijamii.

Kutokana na hali hiyo, ameitaka TANESCO kuzingatia mazingira halisi ya wananchi na kuendelea kutumia gharama ya Shilingi 27,000 ya kuunganisha umeme inayotumika maeneo ya vijijini kwa wananchi wanaostahili utaratibu huo.

“Wananchi hawa wanaoitwa mji mdogo, niwaelekeze watu wa TANESCO, umeme waendelee kuunganishiwa kwa 27,000 ile ile ya kijijini,” amesema Dkt. Mwigulu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi wa Bagamoyo kuwa hati ya urasimishaji wa eneo hilo itapatikana wiki ijayo, akieleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameshafanya uamuzi na kinachosubiriwa ni kukamilishwa kwa taratibu zilizobaki.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha wananchi wanapata hati hiyo ndani ya mwezi huu, hatua inayotarajiwa kusaidia kutatua changamoto za umiliki na urasimishaji wa ardhi katika eneo hilo.

“Mheshimiwa Rais tayari alishakwisha kufanya uamuzi, na mimi niwahakikishie mwezi huu huu, wiki ijayo, mtakuwa mmeshapata hati hiyo,” amesema.

Aidha, Dkt. Mwigulu amemwagiza Kamishna wa Ardhi kufika mwenyewe Bagamoyo kuongoza kliniki maalumu ya kusikiliza na kushughulikia kero za ardhi zinazowakabili wananchi.

Ameelekeza kliniki hiyo kuanza Jumatatu ijayo na kuendeshwa kwa wiki nzima, huku Kamishna huyo akitakiwa kuambatana na timu kutoka makao makuu na kushirikiana na wataalamu wa mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Kamishna wa Ardhi anapaswa kuhudhuria mwenyewe ili kusikiliza malalamiko ya wananchi mmoja mmoja na kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi.

“Usitume mwakilishi, uje mwenyewe kusikiliza mtu mmoja mmoja wewe mwenyewe,” amesisitiza.

Maelekezo hayo yanahusu upatikanaji wa huduma ya umeme kwa gharama inayozingatia mazingira ya wananchi, kukamilishwa kwa urasimishaji wa Bagamoyo na kuimarishwa kwa utatuzi wa migogoro na kero za ardhi katika eneo hilo.

Leave a Comment