KILIMANJARO: Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka Athumani Mbuti, mkazi wa Kijiji cha Mvule, Wilaya ya Same, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Abubaswati Shaban Mbawala, mwenye umri wa miaka 26.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Oktoba 16, 2026, tukio hilo limetokea Oktoba 15, 2026, majira ya saa 8:00 asubuhi katika Kitongoji cha Mapalakanga, Kijiji cha Mvule, Kata ya Kihurio, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa marehemu alifariki dunia akiwa na majeraha mwilini, huku mtuhumiwa akidaiwa kutoweka na familia yake pamoja na mifugo aliyokuwa akifuga nyumbani kwake baada ya tukio hilo.
Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa huyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Aidha, Jeshi la Polisi limewaomba wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo kuzifikisha katika kituo cha polisi kilicho karibu nao au kutumia njia rasmi za mawasiliano na Jeshi hilo.
Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola katika kupambana na uhalifu na kuhakikisha wahusika wa makosa ya jinai wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

