
Simba SC imetangaza kutokwenda uwanjani kushuhudia mchezo wa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC 15 de Agosto utakaopigwa Oktoba 21, 2026, huku ikiwataka mashabiki wake kuelekeza nguvu katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Oktoba 25, 2026, kwenye Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya michezo hiyo, msemaji wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema uamuzi huo umetokana na FC 15 de Agosto kukataa kuruhusu mashabiki kuhudhuria mchezo wa Oktoba 21, licha ya jitihada zilizofanywa na uongozi wa Simba kuwasiliana na wapinzani hao kupitia njia rasmi.
Ahmed amesema Simba ilijaribu kuwashawishi wapinzani hao kuruhusu mashabiki kuingia uwanjani na hata kuahidi kuwasaidia kutangaza mchezo, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa.

“Baada ya FC 15 de Agosto kukataa mashabiki, tulipata taarifa kwamba wanafanya mpango wa chinichini ili mashabiki wawepo. Msimamo wetu kama Simba ni kwamba hatutakwenda uwanjani, tutasubiri mechi ya tarehe 25,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa mashabiki wa Simba hawapaswi kununua tiketi za mchezo huo iwapo zitauzwa kinyume na msimamo uliowasilishwa awali na FC 15 de Agosto.
Katika hatua nyingine, Ahmed ametangaza kuwa mdhamini mkuu wa Simba, Betway Tanzania, ameandaa tukio maalumu la kuwawezesha mashabiki kuutazama mchezo huo kupitia skrini kubwa katika viwanja vya Mwembe 2-1.
Amesema tukio hilo litakuwa na kiingilio cha bure, huku sharti likiwa ni kila mshiriki kuvaa jezi mpya ya Simba ya msimu huu, ambayo amesema bei yake imeshuka hadi Sh 25,000.
Kwa mujibu wa Ahmed, shughuli hiyo itaanza mapema asubuhi kwa kuonyesha marudio ya Kariakoo Derby iliyochezwa Oktoba 10, kabla ya mashabiki kufuatilia mchezo wa kimataifa wa Simba dhidi ya FC 15 de Agosto.
“Uzuri sisi si wageni wa matukio haya ya big screen. Tutafunga skrini kubwa ya kisasa na pamoja na jua la saa tisa alasiri, mashabiki wataona vizuri kutokana na ukubwa wa skrini hiyo,” amesema.
Ameeleza kuwa burudani itakayoambatana na tukio hilo itahusisha DJ Sinyorita, Samio Love, King Faida na kundi lake, pamoja na wasanii wa muziki wa singeli Msaka Daily na Mczo Morfan.
Pia kutakuwa na michezo mbalimbali yenye zawadi, ikiwemo jezi mpya ya Simba iliyosainiwa na mchezaji Elie Mpanzu.
Ahmed amewataka mashabiki kutembelea kurasa za mitandao ya kijamii za Betway, kufuatilia kurasa hizo na kuandika kuwa watahudhuria tukio hilo, huku wakipendekeza majina ya wachambuzi wanaotaka washiriki katika uchambuzi wa mchezo.
Akizungumzia mchezo wa Oktoba 21, Ahmed amesisitiza kuwa Simba haitakiwi kuichukulia FC 15 de Agosto kwa urahisi, akieleza kuwa wapinzani hao wana dhamira kubwa ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Amesema kucheza nyumbani pekee hakumaanishi Simba itapata ushindi, bali maandalizi, ubora wa kikosi na namna wachezaji watakavyojituma ndivyo vitakavyoamua matokeo.
“Matokeo yoyote ya mechi ya kwanza yasitupe uhakika wa kwenda makundi. Wapinzani wetu nao wanataka makundi, ndiyo maana tunapaswa kujiandaa vizuri na kupambana,” amesema.
Ameongeza kuwa Simba imejenga kikosi chenye malengo makubwa zaidi ya ushindi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, akisisitiza kuwa lengo ni kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
“Hatujasajili kwa ajili ya kumfunga Yanga pekee, tumesajili kucheza mpaka hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni bora dunia iishie hapa kuliko Mnyama kushindwa kwenda hatua ya makundi,” amesema Ahmed.
Kwa upande wa mchezo wa Oktoba 25, Ahmed amesema Simba inataka kuona mashabiki wengi wakijitokeza katika Uwanja wa Uhuru ili kuipa timu sapoti katika hatua hiyo muhimu ya mashindano.
Amesema klabu itatangaza viingilio vya mchezo huo kabla ya kuanza kwa mauzo ya tiketi baada ya mchezo wa Oktoba 21.
Ahmed amewakumbusha mashabiki kuwa msimu uliopita walifuatilia mchezo wa kufuzu hatua ya makundi wakiwa Coco Beach, lakini mwaka huu lengo ni kuujaza Uwanja wa Uhuru wenye uwezo wa kuchukua takribani mashabiki 19,000.
“Kwa muda mrefu, ukiachilia mbali mechi dhidi ya Nkana, hatujajaza uwanja kwenye mchezo wa kufuzu makundi. Mwaka huu tunataka tuujaze Uwanja wa Uhuru. Uwanja wa watu 19,000 unatushindaje?” amehoji.
Naye Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru, amewashukuru mashabiki kwa ushirikiano wao, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika tukio la kuangalia mchezo kupitia skrini kubwa na kutumia fursa hiyo kununua tiketi za mchezo wa Oktoba 25.
Simba sasa inaelekeza nguvu katika maandalizi ya michezo hiyo miwili, huku ikilenga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupata sapoti kubwa ya mashabiki wake katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru.