×

Padri Afariki Baada ya Kuangukiwa na Msalaba Akiendesha Misa – Video


Padri Patricio Alfredo Sánchez Molinari amefariki dunia usiku wa Jumamosi, Oktoba 17, 2026, baada ya kuangukiwa na msalaba mkubwa wa mbao wenye sanamu ya Yesu Kristo alipokuwa akiendesha ibada ya Misa Takatifu nchini Ecuador. Tukio hilo limetokea katika Kanisa la Nuestra Señora del Perpetuo Socorro, jijini Guayaquil, na kusababisha taharuki miongoni mwa waumini waliokuwa wakishiriki ibada hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa, padri huyo alikuwa akiongoza misa iliyokuwa ikirushwa mubashara kupitia mitandao ya kijamii wakati msalaba uliokuwa ukining’inia ukutani nyuma ya madhabahu ulipojitoa ghafla na kumwangukia. Tukio hilo lilinaswa kwenye matangazo hayo, huku waumini wakisikika wakipiga mayowe na kujaribu kumsaidia.

Mashuhuda walionekana wakikimbilia eneo la madhabahu mara baada ya msalaba kumwangukia padre huyo. Baadhi ya waumini waliomba msaada wa haraka, huku hali ya taharuki ikitawala kanisani. Taarifa zilizochapishwa hazikutoa maelezo ya kina kuhusu hatua za matibabu alizopatiwa kabla ya kuthibitishwa kwa kifo chake.

Jimbo Kuu Katoliki la Guayaquil lilithibitisha kifo cha Padri Sánchez Molinari kupitia taarifa rasmi, likieleza masikitiko yake kutokana na msiba huo. Taasisi hiyo ilitoa pole kwa familia ya kidini ya Redemptorists, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, huku ikiwaomba waumini kumuombea apumzike kwa amani.

Padri Sánchez Molinari alikuwa paroko wa Kanisa la Nuestra Señora del Perpetuo Socorro na mwanachama wa Shirika la Redemptorists, linalojihusisha na huduma za kiroho na uinjilishaji. Alikuwa akihudumia waumini wa eneo hilo, huku misa zake zikitangazwa pia kupitia mitandao ya kijamii ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Hadi taarifa za awali zilipochapishwa, mamlaka za Kanisa hazikuwa zimeeleza chanzo cha msalaba huo kujitoa ukutani wala kama kulikuwa na hitilafu katika mfumo uliokuwa umeushikilia. Tukio hilo limeibua huzuni kubwa miongoni mwa waumini nchini Ecuador na nje ya nchi, huku video ya tukio hilo ikisambaa katika mitandao ya kijamii.

Leave a Comment