×

Video: Askari 13 Wakamatwa kwa Tuhuma za Vifo vya Watu Wanne Kagera


Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia askari wa Wanyamapori (TANAPA), askari wa Maliasili (TFS), sita na askari Mgambo wanne kwa tuhuma za mauaji ya watu wanne yaliyotokea katika Kijiji cha Kanyamika, Kata ya Karambi, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, tukio hilo lilitokea Oktoba 17, 2026, majira ya saa 10:00 alfajiri katika maeneo ya Kanyamika, barabara kuu ya Muleba kuelekea Biharamulo, ambapo askari hao walikuwa doria katika pori la hifadhi ya Misitu ya Ruiga.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa askari hao walikuwa wakitumia gari lenye namba za usajili 02 JU 354 aina ya Toyota Land Cruiser, lililoendeshwa na dereva askari wa Wanyamapori, TNP. SRIII 3585, Mituni Haji, mwenye umri wa miaka 26.

Wengine waliokuwa kwenye doria hiyo ni pamoja na askari Faustin William Mboko (25), Kingmar Mewama (40), Fluomena Romani France (28), Erick David Muya (25), Yusuph Idd Kwewa (26), Emmanuel Sheki Zabron (25), Yusto David (22), Josiah Msafiri Mahenge (26), Farouk Bashiru Mahamudu (24), Baraka Sadoki Kabulo (28), Regan Bwemelo Nikodem (24), Alanus Beyanga Chowe (35) na Andrew Charles Kwiyega (32), ambaye ni dereva wa TFS.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, askari hao wanadaiwa kuwashambulia kwa risasi watu waliokuwa wamebeba mkaa kwenye pikipiki 10, baada ya watu hao kukataa kusimama walipoamriwa na askari hao. Tukio hilo lilisababisha vifo vya watu wanne.

Watu waliofariki wametajwa kuwa ni Osward Yuster (38), mkazi wa Ngote; Pius Charles (40), mkazi wa Magata; Charles Michael (35), mkazi wa Ngote; na Edgar Elias Lukangula (44), mkazi wa Butembo, ambaye alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera Oktoba 18, 2026, majira ya alfajiri.

Aidha, katika tukio hilo, gari la Serikali mali ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), lenye namba za usajili 02 JU 0354 aina ya Toyota Land Cruiser, liliharibiwa vioo vya mbele na vya pembeni.

Jeshi la Polisi lilieleza kuwa baada ya tukio hilo, lilifanikiwa kukamata pikipiki 10, mkaa magunia 22, mapanga matano, kofia ngumu mbili, makoti mawili, silaha tatu aina ya AK-47, maganda ya risasi 45 pamoja na gari moja aina ya Toyota Land Cruiser mali ya TFS.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limesema limechukua hatua kushughulikia tukio hilo na kuwakamata watuhumiwa wote kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Aidha, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa wananchi kuheshimu sheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi pale wanapokutana na askari au mamlaka zilizopewa dhamana ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi.

Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera.

Nisahihishie idadi ya watuhumiwa na makundi yao

Leave a Comment