
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limeendelea kutoa elimu kwa wananchi na makundi mbalimbali kupitia Falsafa ya Polisi Jamii, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu unaoendelea kuathiri mkoa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Oktoba 19, 2026, kuanzia Septemba 19 hadi Oktoba 18, 2026, jeshi hilo lilifanya misako na operesheni mbalimbali katika maeneo tofauti na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 18 kwa tuhuma za unyang’anyi, huku wengine wakikamatwa kwa tuhuma za wizi wa mifugo, kuvunja na kuiba, utengenezaji wa pombe haramu ya gongo na kujihusisha na magendo.
Katika operesheni hizo, simu za mkononi 34 na pikipiki 24 zilikamatwa kama vielelezo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Aidha, baada ya kesi mbalimbali kufikishwa mahakamani, watuhumiwa 25 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali. Miongoni mwao ni Sufiani Jengo Hamad, aliyehukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kupatikana na mirungi yenye uzito wa kilogramu 109.65.
Mtuhumiwa mwingine, Rashidi Yusuph Mhanga, alihukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji, huku Matano Juma Muro akihukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kusafirisha mirungi.
Katika hukumu nyingine, Ally Juma Mussa, maarufu kama Babu Ally, alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la ubakaji na kulawiti mtoto wa miaka minne. Hukumu hizo ziliamriwa kutumika kwa pamoja.
Vilevile, watuhumiwa 20 walihukumiwa vifungo mbalimbali kwa makosa ya wizi wa mifugo, kuua bila kukusudia, wizi na kuvunja na kuiba.
Kwa upande wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya, operesheni zilizofanyika zilifanikiwa kukamata mirungi kilogramu 46, bangi misokoto 48 na pakiti nne, pamoja na heroin gramu nne. Watuhumiwa hao wanaendelea kuchunguzwa ili hatua nyingine za kisheria zichukuliwe.
Katika kudhibiti makosa ya usalama barabarani, operesheni zilizofanyika ziliwezesha kukamata pikipiki 810 kutokana na makosa mbalimbali, yakiwemo kuendesha bila leseni, kutovaa helmeti, kutokuwa na bima na kupakia mishikaki. Katika operesheni hizo, madereva 340 waliandikiwa faini kwa makosa ya usalama barabarani.
Sambamba na operesheni hizo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limeendelea kuhamasisha wananchi kusalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha sheria. Jumla ya gobore 72 zilisalimishwa hadi Oktoba 18, 2026, huku zoezi hilo likiendelea hadi Oktoba 31, 2026.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limeendelea kutoa wito kwa wananchi kushirikiana nalo katika kuelimishana kuhusu masuala ya usalama, kuimarisha amani na usalama wa jamii, kubaini na kuzuia vitendo vya kihalifu, pamoja na kutoa taarifa ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe kwa wakati.
Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga.