
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa adhabu mbalimbali kwa klabu za Simba SC, TMA FC na Rhino Rangers kutokana na makosa yaliyotokea katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Championship.
Simba imeipiga faini ya jumla ya Shilingi milioni 15 kutokana na makosa mawili yaliyofanywa na mashabiki wake katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Young Africans.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB iliyotolewa Oktoba 22, 2026, Simba imepigwa faini ya Shilingi milioni 10 kwa kosa la mashabiki wake kurusha chupa uwanjani, tukio lililotokea mara kadhaa katika mchezo huo wa watani wa jadi.
Aidha, klabu hiyo imepigwa faini nyingine ya Shilingi milioni tano baada ya mashabiki wake kuvamia eneo la kuchezea wakati mchezo ukiendelea, ambapo mmoja wao alimfuata kijana aliyekuwa akikusanya mipira (Ball Kids) na kumfanyia fujo, kitendo kilichozuiwa na walinzi wa uwanja.
Katika Ligi ya Championship, klabu ya Mbuni FC imepewa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kigamboni United baada ya timu hiyo kushindwa kufika uwanjani kwa sababu zilizotajwa kuwa za msiba na zinazokubalika, hivyo mchezo kushindwa kufanyika.
Vilevile, IAA SC imepewa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rhino Rangers baada ya mtunza vifaa wa Rhino Rangers, Juma Rajab, kuonekana akifanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina wakati timu zikifanya mazoezi ya kujiandaa na mchezo.
Kwa upande mwingine, TMA FC ya Iringa imepewa adhabu kali baada ya kushindwa kufika uwanjani kwa ajili ya mchezo dhidi ya Stand United ya Shinyanga katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, bila sababu za msingi.
Kutokana na kosa hilo, TMA FC imepigwa faini ya Shilingi milioni 10, kutakiwa kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo pamoja na kupokonywa alama tatu na kufungwa mabao matatu katika msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.
Pia, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Twaha Abdallah, amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na klabu yake kushindwa kufika uwanjani kwa ajili ya mchezo huo.
TPLB imesisitiza kuwa adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni za mashindano husika, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha nidhamu, usalama na uadilifu vinaendelea kuzingatiwa katika soka la Tanzania.
