
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa mitihani maalum na mitihani ya marudio imefutwa chuoni hapo, kikisisitiza kuwa taarifa hizo si za kweli.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 23, 2026, na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Prof. Rose A. Upor, UDSM imeeleza kuwa mitihani maalum na mitihani ya marudio bado ipo na itaendelea kutolewa, isipokuwa muda wa kuifanya umebadilika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ili kuongeza ufanisi wa kitaaluma, mitihani hiyo sasa itafanyika ndani ya kalenda ya kawaida ya kitaaluma ya chuo hicho.
UDSM imefafanua kuwa mabadiliko hayo yataathiri ratiba ya mitihani pekee, bila kubadilisha vigezo vya kuendelea na masomo au viwango vya mitihani.
Aidha, chuo hicho kimesisitiza kuwa masharti mengine yote ya mitihani, yakiwemo masharti ya Wastani wa Alama za Kitaaluma (GPA), hayajabadilika na yataendelea kutumika kwa mujibu wa kanuni za mitihani za chuo hicho.
Katika hatua nyingine, wanafunzi wametakiwa kuzingatia masharti ya kozi zao na kuwasiliana na vitengo vyao vya kitaaluma husika ili kupata mwongozo kuhusu hali zao za mitihani, upatikanaji wa kozi na taratibu za kukamilisha mitihani zilizosalia.
Chuo hicho kimewataka wananchi, hususan wanafunzi, kupuuza taarifa hizo za upotoshaji na kupata taarifa sahihi kupitia njia rasmi za mawasiliano za UDSM, ikiwemo tovuti ya chuo hicho, www\.udsm.ac.tz.
Taarifa hiyo imetolewa na Prof. Rose A. Upor, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, tarehe 23 Oktoba 2026.
