×

Gwajima Akemea Matumizi Mabaya ya Mitandao kwa Wanafunzi – Video

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amekemea vikali mwenendo wa baadhi ya mabinti wanafunzi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii, kufuatia video iliyosambaa ikiwaonesha wakiwa wamevaa sare za shule huku wakitamka maneno yasiyofaa wakati wa kusherehekea kuhitimu kidato cha nne.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Dkt. Gwajima ameeleza kusikitishwa na tukio hilo, akitaka kufahamu shule wanazosoma mabinti hao ili suala hilo lifuatiliwe kwa kushirikiana na walimu pamoja na wazazi wao.

“Haya, hawa ni wa shule gani ili tulitendee jambo hili pamoja na walimu wao na wazazi wao? Maana naona wanajiandalia ajali ya maisha yao bila bima,” ameandika Dkt. Gwajima.

Waziri huyo ameongeza kuwa inasikitisha kuona baadhi ya vijana, hususan mabinti, wakigeuza vitendo anavyoviona kuwa havina maadili kuwa mtaji wa kujitafutia maendeleo na ustawi wa maisha.

“Kifupi, huu ni ujinga na ni huzuni sana kuona mabinti kama hawa wakigeuza ujinga kuwa mtaji wa maendeleo na ustawi,” ameongeza.

Kufuatia video hiyo kuzua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, mabinti waliohusika wamejitokeza kupitia video nyingine na kuomba msamaha kwa walimu wao, Watanzania kwa ujumla, Dkt. Gwajima pamoja na Serikali, kutokana na lugha isiyofaa waliyoitumia.

Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii miongoni mwa vijana, hususan wanafunzi, pamoja na nafasi ya wazazi na walimu katika kuwaongoza vijana kuzingatia maadili na kufanya maamuzi yenye manufaa kwa maisha yao ya baadaye.

Leave a Comment