
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amekanusha madai ya upotoshaji kuhusu makadirio ya Shilingi bilioni 730 yaliyotajwa katika Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akifafanua kuwa kiasi hicho si fedha mpya zilizotengwa na Serikali kuu pekee.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Oktoba 25, 2026, Msigwa amesema kiasi hicho ni makadirio ya jumla ya rasilimali zinazotarajiwa kutumiwa na taasisi za Serikali, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa katika kujiandaa na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na El Niño.
Amesema kuwa Shilingi bilioni 730 hazimaanishi fedha taslimu zilizotengwa upya na Serikali kwa ajili ya kugawanywa, bali zinajumuisha bajeti na rasilimali zilizopo katika taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya majanga.
Msigwa amefafanua kuwa taasisi za umma na sekta binafsi zinaendelea kutumia bajeti zao za kawaida zilizoidhinishwa kuimarisha maandalizi, ikiwemo kuchukua hatua za kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Katika hatua nyingine, Msigwa ametoa ufafanuzi kuhusu maana ya El Niño, akieleza umuhimu wa wananchi kuzingatia taarifa za kitaalamu zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu mwenendo wa hali ya hewa na athari zake zinazoweza kujitokeza.
Amesema utabiri wa hali ya hewa ni nyenzo muhimu katika kupanga hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, hivyo amewataka wananchi kuepuka kusambaza taarifa zisizo sahihi na badala yake kufuatilia taarifa kutoka kwenye vyanzo rasmi.
Msigwa amesisitiza kuwa uhuru wa kujieleza na kukosoa upo, lakini ni muhimu mijadala kuhusu masuala ya kitaalamu kuzingatia ukweli na taarifa zinazotolewa na wataalamu wa sekta husika.
Kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na El Niño, amesema maandalizi ya Serikali yanalenga kupunguza hatari ya mafuriko, maporomoko ya ardhi na milipuko ya magonjwa inayoweza kuhusishwa na hali mbaya ya hewa.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka kipaumbele katika kulinda maisha ya wananchi, usalama wao na mali zao kwa kuimarisha mifumo ya tahadhari na utayari wa kukabiliana na majanga.
Msigwa amesisitiza kuwa makadirio ya Shilingi bilioni 730 yanapaswa kueleweka kama jumla ya rasilimali zinazokadiriwa kutumika katika maandalizi ya kukabiliana na majanga, badala ya kutafsiriwa kama fedha mpya zilizotolewa na Serikali kwa matumizi hayo pekee.