
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Watanzania, hususan vijana, kujiepusha na hamasa za uchochezi na kushiriki katika matukio yenye viashiria vya vurugu na uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Oktoba 25, 2026, Msigwa amesema amani na utulivu ni misingi muhimu inayowezesha wananchi na Serikali kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, biashara za ndani na nje ya nchi, pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema mazingira ya amani yana nafasi kubwa katika kukuza uchumi na kuboresha ustawi wa jamii, hivyo ni muhimu kwa kila Mtanzania kulinda utulivu wa nchi na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.
Akizungumzia madai na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, Msigwa ameeleza kuwa Serikali ina mifumo rasmi na sheria zinazopaswa kutumiwa katika kushughulikia malalamiko na kutafuta suluhisho la matatizo yanayojitokeza katika jamii.
Amesisitiza kuwa vurugu, uchochezi na kuchocheana hasira si njia sahihi za kutatua changamoto, bali zinaweza kuhatarisha misingi ya umoja na amani iliyojengwa nchini.
“Madai mbalimbali ya wananchi hayatatuliwi kwa vurugu, kwa kuchocheana, kwa kutiana hasira na kuharibiana misingi na tunu ya nchi yetu. Naomba kutoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kujiepusha kushiriki katika matukio yoyote yenye viashiria vya vurugu na uvunjifu wa amani,**” amesema Msigwa.
Aidha, Msigwa amesisitiza kuwa jukumu la kulinda amani ni la Watanzania wenyewe, akionya kuwa nchi inapokumbwa na machafuko, juhudi za wananchi katika kurejesha utulivu huwa muhimu sana.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kupuuza hamasa zinazoweza kusababisha machafuko na badala yake kutumia njia zilizowekwa kisheria kuwasilisha madai yao na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria na kulinda amani na utulivu ili kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi, kijamii na maendeleo ya taifa.
Amani ni msingi wa maendeleo, na kulinda utulivu wa nchi ni jukumu la kila Mtanzania.