×

Nicki Minaj Aungana na Trump Jukwaani, Awahamasisha Wamarekani

Rapa maarufu duniani, Nicki Minaj, amemuunga mkono Rais wa Marekani, Donald Trump, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Michigan siku ya Jumapili, akisema kiongozi huyo amebadilisha hali ya kisiasa na matumaini ya wananchi nchini humo.

Minaj alijiunga na Trump katika mkutano huo kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula unaotarajiwa kufanyika Novemba 3, 2026, huku akiwahimiza wapiga kura kuwaunga mkono wagombea wa Chama cha Republican.

Akizungumza baada ya Trump kumkaribisha jukwaani na kumsifu, Minaj alisema Rais huyo amewapa Wamarekani matumaini ya kutazamia maisha bora zaidi ya baadaye.

“Amewapa mustakabali ambao tunaweza kuutazamia kwa matumaini. Tunahitaji watu hawa wote wazuri wachaguliwe, kwa sababu huu ni wakati muhimu wa mabadiliko kwa nchi yetu,” alisema Minaj.

Rapa huyo aliyezaliwa nchini Trinidad na Tobago aliwahi kujitambulisha kama shabiki mkubwa wa Trump, akieleza msimamo wake wa kumuunga mkono rais huyo wa Marekani.

Katika mkutano uliofanyika Port Huron, Michigan, Minaj alivutia umati akiwa amevalia suti ya rangi ya dhahabu yenye nembo ya Gucci. Pia aliongoza umati wa watu katika kaulimbiu za kumshangilia Trump na wagombea wa Republican katika jimbo hilo.

Trump, ambaye alimwalika Minaj jukwaani, alimsifu rapa huyo alipokuwa akiondoka, akisema hajawahi kuonekana mrembo zaidi na kuongeza kuwa ni mwanamke mwenye akili anayeelewa mambo.

Kabla ya mkutano huo, Minaj alisafiri pamoja na Trump ndani ya ndege ya rais wa Marekani, Air Force One. Akiwa ndani ya ndege hiyo, alirekodi video ya utani akifanya mahojiano ya kuigiza na msaidizi wa Trump, akijifanya mgombea wa nafasi ya msemaji wa Ikulu ya White House. Video hiyo baadaye iliwekwa

Jimbo la Michigan ni miongoni mwa maeneo yanayofuatiliwa kwa karibu kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula, kutokana na ushindani mkali kati ya wagombea wa vyama vikuu vya Marekani.

Katika kinyang’anyiro cha Seneti, mgombea wa Democratic, Abdul El-Sayed, anakabiliwa na mpinzani wake wa Republican, Mike Rogers.

Kwa upande mwingine, Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, alifanya kampeni pamoja na El-Sayed katika mkutano uliofanyika Jumamosi, siku moja kabla ya Trump kuungana na Minaj katika kampeni za Republican.

Ushiriki wa Minaj katika kampeni hizo unaongeza mjadala kuhusu nafasi ya watu maarufu katika siasa za Marekani, hasa wakati wagombea wakitafuta uungwaji mkono wa wapiga kura kuelekea uchaguzi wa Novemba 3.

Leave a Comment