
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amempongeza mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kusimamia utekelezaji wa maono ya kuhamishia makao makuu ya Serikali jijini Dodoma, akisema hatua hiyo imesaidia kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Rais Samia amesema uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali ni sehemu ya maono ya muda mrefu ya Mwalimu Nyerere, ambaye alitamani kuona makao makuu ya nchi yakihamishiwa katikati ya Tanzania ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuleta maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza leo, Oktoba 30, 2026, wakati wa uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Rais Samia amesema Watanzania wanapaswa kujivunia mafanikio hayo na kutambua mchango wa marais na viongozi mbalimbali waliohusika katika kufanikisha azma hiyo.
Mji wa Serikali Mtumba umejengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 700, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika kuimarisha shughuli za kiutawala nchini.

Amesema dhamira ya kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma ilikuwa ni kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kupunguza gharama na usumbufu wa kuzifuata huduma hizo.
Hata hivyo, amefafanua kuwa Serikali haiwalazimishi wananchi kusafiri hadi Dodoma ili kupata huduma, bali inaendelea kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwawezesha kupata huduma za Serikali kwa njia za kidijitali popote walipo.

Aidha, Rais Samia amesema kuhamia kwa shughuli za Serikali jijini Dodoma kumechochea ukuaji wa jiji hilo kwa kuongeza idadi ya watu, shughuli za biashara, uwekezaji na upatikanaji wa huduma mbalimbali.
Ameongeza kuwa mabadiliko hayo yamefungua fursa nyingi za kiuchumi na kijamii kwa wananchi, ikiwemo biashara za vifaa vya ujenzi, huduma mbalimbali pamoja na uwekezaji katika sekta ya nyumba na majengo ya biashara.

“Serikali, sekta binafsi na wananchi wameongeza ujenzi wa majengo ya kisasa ya makazi, biashara na utoaji wa huduma mbalimbali,” amesema Rais Samia.
Mafanikio hayo yanaendelea kuifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha shughuli za Serikali, biashara na uwekezaji, huku yakidhihirisha mwendelezo wa utekelezaji wa maono ya viongozi waliotangulia katika kulijenga taifa.