×

Benki ya Equity na Reforest Africa Washirikiana Kupanda Miti 6,500

Benki ya Equity Tanzania, kwa kushirikiana na Reforest Africa, asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na urejeshaji wa misitu na uhifadhi wa mazingira, wametekeleza mpango wa pamoja uliolenga kurejesha mazingira, kuhifadhi misitu na kuwezesha jamii kiuchumi kupitia upandaji miti na utoaji wa elimu ya fedha katika eneo la Mang’ula, Kilombero, mkoani Morogoro.

Mpango huo uliunganisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na uwezeshaji wa jamii, ukiakisi dhamira ya Benki ya Equity ya kuchangia maendeleo endelevu na kupanua fursa za kiuchumi kwa jamii.

Ushirikiano huo pia uliunga mkono juhudi za Reforest Africa za kurejesha misitu iliyoharibika, kulinda makazi ya wanyamapori na kushirikisha jamii katika utunzaji wa rasilimali za asili, hususani katika maeneo ya Kilombero na Udzungwa.Shughuli zilianza kwa zoezi la upandaji miti katika Msitu wa Magombera.

Katika awamu ya kwanza, miche 1,000 ya miti ya asili ilipandwa kuelekea lengo la jumla la miti 6,500 Zoezi hilo lililenga kuchangia urejeshaji wa makazi asilia na kulinda ukanda wa tembo kupitia upandaji wa miti inayofaa kwa mazingira husika.

Upandaji wa miche iliyobaki ulipangwa kuendelea hadi mwisho wa mwaka, kwa kuzingatia hali ya hewa na mazingira yanayofaa kwa ukuaji wa miti.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Jasto Msimiyungu, Katibu Tarafa wa Mang’ula na Mgeni Rasmi, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za kifedha, mashirika ya uhifadhi wa mazingira, viongozi na wananchi katika kulinda rasilimali za asili na kuchochea maendeleo endelevu ya jamii.

“Uhifadhi wa mazingira ni jukumu la pamoja linalohitaji ushiriki wa kila mmoja wetu. Tunapaswa kulinda misitu yetu na makazi ya wanyamapori kwa manufaa ya jamii zetu na vizazi vijavyo.

Ninaipongeza Benki ya Equity Tanzania na Reforest Africa kwa kuunganisha juhudi za upandaji miti na elimu ya fedha, kwa kuwa maendeleo ya jamii yanahitaji mazingira endelevu pamoja na wananchi wenye maarifa na uwezo wa kujiletea maendeleo,” alisema Bw. Msimiyungu.

Kwa upande wake, Bi. Hellen Dalali, Mkuu wa Uendelevu wa Benki ya Equity Tanzania, alisema kuwa ushirikiano huo unaonesha dhamira ya Benki ya kuendeleza mipango inayochangia uhifadhi wa mazingira sambamba na kuimarisha ustawi wa kiuchumi wa jamii.

“Tunaamini kuwa maendeleo endelevu yanahitaji jamii zenye uwezo wa kiuchumi na mazingira salama yatakayohakikisha ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kupitia ushirikiano wetu na Reforest Africa, tunachangia juhudi za kurejesha misitu na kuhifadhi mazingira, huku tukitoa elimu ya fedha inayowawezesha wanawake na vijana kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kukuza shughuli zao za kiuchumi na kunufaika na fursa zinazopatikana kupitia huduma rasmi za kifedha,” alisema Bi. Dalali aliongeza kuwa Benki ya Equity inaendelea kuwekeza katika mipango ya uendelevu inayounganisha uhifadhi wa mazingira, uwezeshaji wa jamii na upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha, kwa kutambua kuwa mazingira salama na uchumi imara ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu.

Baada ya zoezi la upandaji miti, Benki ya Equity chini ya dirisha la Mwanamke Plus ilitoa mafunzo ya elimu ya fedha katika Shule ya Msingi Mang’ula A.

Mafunzo hayo yalilenga wanawake na vijana, yakijumuisha masuala ya kuweka akiba, kupanga bajeti, usimamizi wa fedha binafsi na biashara, ukuaji wa biashara na uelewa wa huduma rasmi za kifedha. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea washiriki uwezo wa kusimamia rasilimali zao za kifedha na kutumia huduma za kifedha kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Mafunzo hayo yamewafikia washiriki zaidi ya 150, wakiwemo wanawake, vijana, pamoja na wanajamii wengine.

Kupitia ushirikiano na Reforest Africa, Benki ya Equity Tanzania inaendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo endelevu kwa kuhimiza utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha na uwezeshaji wa jamii ili kujenga mustakabali bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Benki ya Equity inaendelea kuwawezesha wanawake wajasiriamali na vijana kwa kushughulikia mahitaji yao ya kibenki na kuhakikisha ushiriki wao kamili katika ukuaji wa uchumi.

Benki inaelewa changamoto ambazo wanawake hupitia kifedha, hivyo imetengeneza suluhisho za kipekee chini ya dirisha la Mwanamke Plus ikiwemo ufadhili wa 100% kwa aina zote za biashara na nyumba bila hitaji la mchango wa awali wa 30%,dhamana ya mkopo hadi 70% ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa biashara za wanawake,mafunzo bure ya elimu ya kifedha na ujasiriamali kwa vikundi au matukio ya wanawake na vijana, mikopo nafuu ya kununua mashine za kushona na vifaa vya ushonaji chini ya Ushonaji Plus Pamoja . Kwa wateja na wadau wanaotaka kufahamu zaidi kuhusu Huduma za Benki  na suluhisho nyingine za kifedha za Equity Bank Tanzania, wanakaribishwa kutembelea tawi la Equity lililo karibu nao, kuwasiliana kupitia 0768985500

Kuhusu Benki ya Equity Tanzania

Equity Bank Tanzania Limited ni benki ya biashara yenye makao makuu katika Golden Jubilee Towers, Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam.

Kwa maelezo zaidi kuhusu habari hii, tafadhali wasiliana na:

Shumbana Walwa |  Equity Bank Tanzania Limited | Simu: +255 689 737 122  |  Barua pepe: [email protected]

Leave a Comment