
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameagana na viongozi mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, leo Novemba 10, 2026, kabla ya kuanza safari ya kuelekea jijini Antalya, Uturuki.
Rais Samia anakwenda nchini humo kushiriki Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaowakutanisha viongozi wa mataifa mbalimbali pamoja na wadau wa mazingira kutoka sehemu tofauti duniani.

Katika mkutano huo, viongozi wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mabadiliko ya tabianchi, athari zake kwa mazingira na maisha ya wananchi, pamoja na mikakati ya kimataifa ya kukabiliana na changamoto hizo.
Aidha, Rais Samia anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (Antalya Leaders’ Summit), pamoja na kikao cha ngazi ya juu kinachohusu matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni sehemu ya mijadala ya kimataifa kuhusu juhudi za kulinda mazingira, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

