×

Mwigulu Aagiza Takukuru Kuchunguza Miradi Inayolalamikiwa Shinyanga

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga kufanya uchunguzi wa miradi ya maendeleo inayolalamikiwa kuchelewa kukamilika na kujengwa chini ya kiwango, akitaka taarifa za uchunguzi huo ziwasilishwe moja kwa moja kwake ili hatua stahiki zichukuliwe.

Dkt. Mwigulu alitoa agizo hilo Jumatatu, Novemba 9, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya JASCO, Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, kufuatia malalamiko kuhusu utekelezaji wa miradi ya barabara, stendi na soko kuu.

Alimwelekeza Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha maeneo yote yaliyotajwa na wananchi yanafanyiwa uchunguzi na taarifa zinamfikia moja kwa moja ili kuwezesha hatua za haraka.

“Hebu tusaidie kuangalia maeneo haya ambayo yamelalamikiwa. Na hiyo taarifa niipate mwenyewe ili niweze kuchukua hatua haraka,” alisema Waziri Mkuu.

Alisisitiza kuwa Serikali haitakubali fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kutotumika ipasavyo huku wananchi wakikosa huduma zinazotarajiwa.

“Tutachukua hatua kali tukibaini kuna ubadhirifu wowote ama kuna uzembe umefanyika katika eneo lolote lile,” alionya.

Awali, Mbunge wa Shinyanga Mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, aliwasilisha malalamiko kuhusu kasi ya ujenzi wa stendi pamoja na barabara inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kupitia mradi wa TACTIC.

Katambi pia alieleza wasiwasi kuhusu ubora wa ujenzi wa barabara ya Old Shinyanga–Bubiki, akidai kuwa baadhi ya maeneo yanaonyesha dalili za kuharibika kabla ya kazi za ujenzi kukamilika.

Kuhusu ujenzi wa soko kuu la Shinyanga, aliomba Serikali Kuu kuongeza fedha za kukamilisha mradi huo, akieleza kuwa Manispaa imekuwa ikitumia mapato yake ya ndani kugharamia utekelezaji wake.

Akijibu malalamiko hayo, Dkt. Mwigulu alisema uchunguzi utasaidia kubaini changamoto zilizopo katika miradi hiyo na kuweka msingi wa kuchukua hatua dhidi ya uzembe au ubadhirifu utakaothibitika.

Alisisitiza kuwa viongozi na watendaji wa Serikali katika ngazi zote wana wajibu wa kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wa Shinyanga wanapata manufaa yanayotarajiwa kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali.

MWISHO

Leave a Comment