×

Halmashauri Zahimizwa Kutumia PPP Kutekeleza Miradi ya Maendeleo

Halmashauri nchini zimehimizwa kutumia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) kutekeleza miradi ya kibiashara na huduma za jamii, ikiwemo masoko, vituo vya mabasi, hoteli na miundombinu mingine, badala ya kutegemea fedha za Serikali pekee.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema mfumo huo unatoa fursa kwa halmashauri kutumia mitaji na utaalamu wa sekta binafsi kuendeleza miradi inayoweza kujiendesha kibiashara na kuchangia maendeleo ya maeneo husika.

Akizungumza katika kongamano la uwekezaji mkoani Tanga, Kafulila alisema sheria ya PPP imeweka utaratibu unaorahisisha uandaaji na uidhinishaji wa miradi midogo ya ubia inayotekelezwa na halmashauri.

Alisema miradi hiyo haihitaji kupitia taratibu zote zinazotumika kwa miradi mikubwa ya kitaifa, kwani kwa mujibu wa utaratibu alioueleza, maamuzi ya miradi ya aina hiyo yanaweza kufanywa na mkurugenzi wa halmashauri husika.

“Kwa miradi midogo ya halmashauri, kama ujenzi wa stendi, soko au hoteli, sheria imerahisisha utaratibu ili kuondoa urasimu usio wa lazima. Maamuzi yanaweza kufanywa na mkurugenzi wa halmashauri,” alisema.


Kafulila alisema hakuna sababu ya Serikali kutumia fedha za bajeti kujenga kila soko, kituo cha mabasi au miundombinu mingine ambayo sekta binafsi inaweza kuwekeza na kuiendesha kwa ufanisi.

Alibainisha kuwa sheria pia inatoa nafasi kwa Serikali kuchangia sehemu ya mtaji katika miradi ambayo ina manufaa makubwa kiuchumi na kijamii, lakini mapato yake ya kibiashara hayatoshi kumshawishi mwekezaji binafsi kuitekeleza peke yake.

Alitoa mfano wa mradi wa kituo cha mabasi unaohitaji mtaji wa Sh20 bilioni, lakini tathmini ya kibiashara ikaonesha kuwa mwekezaji anaweza kurejesha gharama za Sh15 bilioni pekee.

Alisema katika mazingira hayo, Serikali inaweza kuchangia Sh5 bilioni ili kuwezesha mradi kutekelezeka na kuwa na manufaa kwa umma pamoja na mvuto wa kibiashara kwa mwekezaji.

Alisema utaratibu huo unasaidia kuunganisha maslahi ya kijamii na kibiashara, huku ukipunguza mzigo wa Serikali wa kugharamia miradi yote kwa kutumia mapato ya kodi.

Kafulila alizitaka halmashauri kujipima kwa idadi na ubora wa fursa za uwekezaji wanazozitengeneza katika maeneo yao, akisema jukumu la viongozi wa Serikali za mitaa kwa sasa ni pamoja na kuvutia biashara na mitaji kwa ajili ya ustawi wa wananchi.

Alisema Serikali inapaswa kuelekeza fedha zake katika maeneo ambayo sekta binafsi haiwezi kuyahudumia kwa ufanisi, ikiwemo kuboresha elimu, afya na huduma nyingine muhimu kwa wananchi.

Aidha, aliwahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani kutumia fursa zinazotolewa na mfumo wa PPP, akisema miradi hiyo haijawekewa nafasi kwa makampuni makubwa pekee.

Alisema kampuni ndogo na vikundi vya wafanyabiashara vinaweza kuungana, kuunganisha mitaji na kushiriki katika miradi inayohitaji uwekezaji wa pamoja.

Alisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza uwekezaji, kupanua shughuli za kiuchumi na kujenga uchumi unaozalisha ajira na kuboresha maisha ya wananchi.

 

Leave a Comment