×

Wapanda Mlima 22 wa ARiS na TIRA Wafika Kilele cha Kilimanjaro Kupitia Kili Insurance Summit 2026

KILIMANJARO, 12 Novemba 2026: Wapanda mlima 22 kutoka ARiS Risk & Insurance Solutions Limited na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), wakipata mwongozo na usaidizi wa uratibu wa safari kutoka kampuni ya Ahsante Tours, wamefanikiwa kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro, chenye urefu wa mita 5,895 juu ya usawa wa bahari, na kurejea salama. Safari hiyo ilikuwa sehemu ya mpango wa Kili Insurance Summit 2026, unaolenga kuadhimisha miaka 30 ya mageuzi ya soko la bima nchini Tanzania.

Kili Insurance Summit 2026 inaongozwa na kaulimbiu isemayo “Miaka 30 ya Ubora katika Sekta ya Bima, Tukifikia Viwango Vipya kwa Pamoja.” Kaulimbiu hii inaunganisha maadhimisho ya miaka 30 ya mageuzi ya soko la bima na ujumbe mpana kuhusu umuhimu wa maandalizi, ushirikiano na ustahimilivu katika kufikia malengo makubwa.

Timu hiyo ilianza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia Lango la Machame tarehe 6 Novemba, ilifika kilele cha Uhuru tarehe 11 Novemba 2026 na kushuka kupitia Lango la Mweka tarehe 12 Novemba. Safari hiyo ilihitaji maandalizi ya kutosha, nidhamu na mshikamano katika kukabiliana na changamoto za mazingira ya mlima.

Akizungumzia mafanikio hayo, Christopher Siara, Meneja Mkuu na Afisa Mkuu wa Bima wa ARiS Insurance, alisema kufika kileleni kwa washiriki wote ni hatua muhimu kwa timu hiyo.

“Tunafurahi kuona wapanda mlima wote 22 wakifanikiwa kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Mafanikio haya yanaonesha umuhimu wa maandalizi, nidhamu na ushirikiano ulioonyeshwa na kila mmoja katika timu. Safari hii imetukumbusha umuhimu wa kujiandaa mapema na kutambua vihatarishi ili tuweze kuchukua hatua sahihi za kukabiliana na changamoto zinapojitokeza”.

“Katika kipindi cha miaka 30 tangu mageuzi ya soko la bima yalipoanza, tumeshuhudia mabadiliko makubwa na fursa mpya za ukuaji wa sekta hii. Tunaamini ni muhimu kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu nafasi ya bima katika kulinda watu, mali na shughuli za kiuchumi, huku tukitumia fursa zilizopo kuimarisha zaidi sekta hii,” alisema Siara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Ahsante Tours, Cuthbert Swai, alisema jukumu la kampuni hiyo lilihusisha kuwaongoza wapanda mlima na kuratibu mahitaji yao katika kipindi chote cha safari.

“Kupandisha timu katika Mlima Kilimanjaro kunahitaji uratibu mzuri, maandalizi ya kutosha na kuzingatia mahitaji ya kila mshiriki. Tunafurahi kuwaongoza na kuwasaidia washiriki kutoka ARiS na TIRA katika safari hii. Mafanikio yao ya kufika kileleni yanaonesha umuhimu wa ushirikiano, nidhamu na kufanya kazi pamoja ili kufikia lengo moja,” alisema Swai.

Kwa upande wa TIRA, Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, alisema safari hiyo imeonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi katika kuendeleza sekta ya bima na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za bima.

“Ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi ni muhimu katika kuendeleza soko la bima. Jitihada za pamoja za wadau zinaweza kusaidia kuongeza uelewa wa wananchi, kupanua upatikanaji wa huduma za bima na kuchochea ukuaji endelevu wa sekta hii nchini kote,” alisema Dkt. Lupilya.

Kabla ya kuanza safari hiyo, washiriki walifanya maandalizi ya kimwili yaliyohusisha mazoezi katika eneo la Pugu, Dar es Salaam, pamoja na safari ya siku mbili katika Milima ya Uluguru mkoani Morogoro.

Kampeni ya Kili Insurance Summit 2026 imejengwa katika dhana ya “Safari ya Kufika Kileleni Haianzi Mlimani,” inayosisitiza kuwa mafanikio huanza na maandalizi. Dhana hii inaangazia umuhimu wa kutambua vihatarishi mapema na kuchukua hatua stahiki za kuvidhibiti. Ujumbe huu unaendana na misingi ya bima na usimamizi wa vihatarishi, ambayo husaidia watu binafsi na taasisi kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza na kujilinda dhidi ya athari zake za kifedha.

Leave a Comment