×

Pochettino Kuiongoza Marekani Katika Mechi Mbili Kabla ya Kujiunga na Man United

MANCHESTER, ENGLAND: Mauricio Pochettino anatarajiwa kuendelea kuiongoza timu ya taifa ya Marekani katika michezo yake miwili ijayo dhidi ya Haiti, licha ya kuhusishwa na nafasi ya ukocha mkuu wa klabu ya Manchester United.

Manchester United haina pingamizi na uwezekano huo, huku mazungumzo kati ya klabu hiyo na Shirikisho la Soka la Marekani (US Soccer) yakitarajiwa kushika kasi ndani ya saa 24 zijazo.

Pochettino, raia wa Argentina, ameripotiwa kufikia makubaliano ya awali ya mdomo ya kuiongoza Manchester United endapo klabu hiyo itaamua kuachana na kocha wake wa sasa, Michael Carrick.

Hata hivyo, United inatambua kuwa kocha huyo bado ana majukumu na timu ya taifa ya Marekani, hivyo inataka kushughulikia suala hilo kwa kuzingatia ratiba yake ya kimataifa.

Miongoni mwa mambo yanayopaswa kukamilishwa kabla ya Pochettino kuhamia Old Trafford ni mazungumzo kuhusu malipo ya fidia ya kuvunja mkataba wake na US Soccer, yanayokadiriwa kufikia pauni milioni saba, pamoja na makubaliano ya kuwaleta pamoja wasaidizi wake wa benchi la ufundi.

Kwa upande mwingine, United inatarajia kurejea kwa wachezaji wake wengi ifikapo Alhamisi ijayo, kabla ya safari ya kwenda Anfield kukabiliana na Liverpool Jumapili, Novemba 22, katika mchezo utakaorushwa mubashara na Sky Sports.

Akizungumzia uwezekano wa Pochettino kujiunga na Manchester United, mwandishi mkuu wa Sky Sports News, Kaveh Solhekol, amesema kocha huyo ana uwezo wa kuboresha kiwango cha timu hiyo kutokana na uzoefu wake wa Ligi Kuu England.

Solhekol amekumbushia mafanikio ya Pochettino akiwa Chelsea, ambapo licha ya timu hiyo kuwa katikati ya msimamo wa ligi kuelekea mwishoni mwa msimu, iliibuka na ushindi katika michezo yake mitano ya mwisho na kumaliza nafasi ya sita.

Hata hivyo, Pochettino aliondoka Chelsea baada ya msimu mmoja pekee, akieleza kuwa kulikuwa na changamoto za kimuundo zilizomzuia kutekeleza kikamilifu mipango yake ya kazi.

Kocha huyo amewahi pia kuinoa Tottenham Hotspur na Paris Saint-Germain, huku akijijengea jina katika soka la Ulaya kutokana na falsafa yake ya uchezaji na uwezo wa kusimamia wachezaji.

Iwapo makubaliano yatafikiwa, Pochettino atakuwa na jukumu la kuiongoza Manchester United katika kipindi muhimu cha msimu, huku mashabiki wakisubiri kuona kama atarejesha ushindani na kiwango cha timu hiyo.

Leave a Comment