×

Ifahamu Concorde, Ndege ya Kifahari Iliyokuwa na Kasi ya Kushangaza Duniani

Concorde ilikuwa ndege ya abiria aina ya Jet iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa wahandisi kutoka Ufaransa na Uingereza katika miaka ya 1950. Ndege hiyo ilikuja kuwa miongoni mwa teknolojia za kipekee kuwahi kutengenezwa katika historia ya usafiri wa anga kutokana na kasi yake kubwa iliyozidi mara mbili ya kasi ya sauti.

Jina Concorde lilitokana na neno lenye maana ya makubaliano, umoja au muungano, likiwakilisha ushirikiano wa mataifa hayo mawili katika ujenzi wa ndege hiyo iliyokuwa na uwezo wa kipekee.

Concorde ilifanya safari yake ya kwanza mwaka 1969 na kuanza safari rasmi za kibiashara mwaka 1976. Iliendelea kutoa huduma kwa takribani miaka 27 kabla ya kustaafu mwaka 2003.

Ndege hiyo ilikuwa na uwezo wa kubeba marubani wawili, mhandisi mmoja wa ndege, wahudumu wengine sita pamoja na abiria kati ya 92 na 128, kutegemea mpangilio wa viti.

Moja ya mambo yaliyowafanya watu wengi kuishangaa Concorde ni uwezo wake wa kusafiri kwa kasi ya Supersonic, ambayo ni kasi inayozidi kasi ya sauti. Ndege hiyo iliweza kufikia Mach 2, sawa na takribani kilomita 2,180 kwa saa.

Ili kuweza kuondoka ardhini, Concorde ilihitaji kufikia kasi ya takribani kilomita 400 kwa saa katika njia ya kurukia ndege. Baada ya kuruka, ilikuwa na uwezo wa kupanda kwa kasi kuelekea kwenye urefu wa safari yake.

Pia, ilikuwa na uwezo wa kusafiri katika urefu wa futi 60,000 kutoka usawa wa bahari, sawa na takribani mita 18,000. Urefu huo ulikuwa juu zaidi ya kiwango kinachotumiwa na ndege nyingi za kawaida za abiria.

Concorde ilikuwa na muundo maalumu wa pua iliyokuwa na uwezo wa kushushwa wakati wa kutua na kuinuliwa wakati wa safari. Teknolojia hiyo ilisaidia marubani kuona vizuri njia ya mbele wakati wa kuendesha ndege ardhini na wakati wa kutua, kutokana na pua yake kuwa ndefu na iliyochongoka.

Kutokana na kasi yake kubwa, ndege hiyo iliweza kusafiri kutoka London nchini Uingereza hadi New York nchini Marekani kwa takribani saa tatu na nusu, tofauti na ndege nyingine ambazo zilihitaji takribani saa nane kukamilisha safari hiyo.

Hali hiyo ilisababisha Waingereza kutumia msemo maarufu wa Kiingereza, “Arrive Before You Leave”, unaomaanisha kufika kabla ya muda wa kuondoka. Msemo huo ulitokana na tofauti ya saa kati ya London na New York, ambapo London iko mbele kwa takribani saa tano.

Hata hivyo, kasi hiyo kubwa ilikuwa na athari zake. Wakati Concorde ikisafiri kwa kasi ya Supersonic, joto lililosababishwa na msuguano na mkandamizo wa hewa lilifanya sehemu za nje ya ndege kufikia nyuzi joto 130 za Selsiasi.

Joto hilo lilisababisha mwili wa ndege kutanuka na kuongezeka urefu kwa takribani inchi sita hadi tisa wakati ikiwa katika kasi ya Mach 2.

Kwa upande wa matumizi ya mafuta, Concorde ilikuwa ikitumia takribani lita 22,000 kwa saa moja. Mafuta hayo yalihifadhiwa katika matenki yaliyokuwa ndani ya mabawa na sehemu nyingine za ndege.

Ndege hiyo pia ilikuwa na mfumo wa kufuatilia mionzi ya anga uliowasaidia marubani kufahamu kiwango cha mionzi wanachokutana nacho wakati wa safari za juu angani na kufanya marekebisho ya urefu wa safari inapohitajika.

Licha ya teknolojia yake ya kipekee, Concorde ilikuwa usafiri wa gharama kubwa uliotumiwa zaidi na watu wenye uwezo mkubwa kifedha. Kwa mfano, mwaka 1997, tiketi ya safari ya kwenda na kurudi kati ya London na New York ilifikia takribani dola za Marekani 7,995 kwa mtu mmoja.

AJALI ILIYOTIKISA HISTORIA YA CONCORDE

Katika historia yake ya huduma za kibiashara, Concorde ilipata ajali moja mbaya iliyotokea Julai 25, 2000, wakati ndege ya shirika la Air France ilipokuwa ikijiandaa kuruka kutoka Paris kuelekea New York.

Wakati wa kukimbia katika njia ya kurukia, ndege hiyo ilipita juu ya kipande cha chuma kilichokuwa kimeanguka kutoka kwenye ndege nyingine iliyokuwa imetangulia kuruka.

Kipande hicho kilisababisha tairi la ndege kupasuka na vipande vyake kurushwa kwa nguvu, vikigonga sehemu ya chini ya bawa na kuharibu mfumo wa mafuta na kusababisha moto mkubwa.

Moto huo ulisababisha ndege kupoteza uwezo wa kuendelea na safari salama na hatimaye kuanguka karibu na hoteli iliyokuwa eneo la Gonesse nchini Ufaransa.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 113, wakiwemo abiria 100, wafanyakazi tisa wa ndege na watu wanne waliokuwa ardhini.

Tukio hilo lilikuwa pigo kubwa kwa historia ya Concorde, ingawa ndege hizo ziliendelea kutoa huduma baada ya kusitishwa kwa safari kwa muda na kufanyiwa maboresho ya kiusalama.

MWISHO WA CONCORDE

Mwaka 2003, huduma za Concorde zilifikia mwisho baada ya changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa za uendeshaji, matengenezo na kupungua kwa mahitaji ya usafiri huo.

British Airways ilifanya safari yake ya mwisho ya kibiashara Oktoba 24, 2003, huku Air France nayo ikiwa imesitisha huduma za ndege hizo mwaka huohuo.

Tangu wakati huo, ndege za Concorde zimehifadhiwa katika makumbusho mbalimbali duniani kama kumbukumbu ya moja ya mafanikio makubwa zaidi ya teknolojia ya usafiri wa anga.

Hadi leo, Concorde inaendelea kuwa miongoni mwa ndege za abiria zinazokumbukwa zaidi duniani kutokana na kasi yake ya ajabu, teknolojia yake ya kipekee na uwezo wake wa kupunguza muda wa safari za masafa marefu.

Makala: Elvan Stambuli, GPL

Leave a Comment