×

Mwanaume Ahukumiwa Maisha Jela Kwa Kumlawiti Mtoto Wa Miaka 10

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi, Novemba 12, 2026, imemhukumu Saidi Mussa Kwakupile, mkazi wa Kijiji cha Mtua mkoani humo, kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka 10.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Magara katika kesi namba 18547/2026, iliyokuwa ikisikilizwa katika mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa maelezo ya kesi, tukio hilo lilitokea Julai 19, 2026, majira ya usiku, ambapo Kwakupile alidaiwa kumvizia mtoto huyo akiwa amelala na kutenda kosa hilo.

Kwakupile alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 19, 2026, na kusomewa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili, ambayo aliyakana.

Katika kuendesha kesi hiyo, upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Hilali Hamza, uliwasilisha mashahidi saba pamoja na vielelezo vitatu mahakamani kwa lengo la kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

Baada ya kusikiliza ushahidi uliowasilishwa na pande husika, mahakama ilimkuta na hatia na kumhukumu kutumikia kifungo cha maisha gerezani.

Leave a Comment