
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameeleza historia ya kuanzishwa kwa huduma za tiba ya dharura nchini Tanzania, akibainisha kuwa hatua hiyo ilitokana na maono ya kuboresha mfumo wa afya na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa wagonjwa mahututi na majeruhi.
Akizungumza katika Mkutano wa Nane wa Tiba ya Dharura Afrika (ACEM 2026), unaofanyika jijini Arusha, Dkt. Kikwete amesema safari ya kuanzishwa kwa huduma hizo ilianza mwaka 2007, kupitia mazungumzo yake na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Abbott Fund, Miles White.
Amesema katika mazungumzo hayo walijadili namna ya kuboresha huduma za afya nchini, ikiwemo kuimarisha huduma za maabara katika hospitali za mikoa pamoja na kuanzisha mfumo bora wa huduma za tiba ya dharura.

Dkt. Kikwete amesema mwaka 2008, Abbott Fund ilijitolea kusaidia maendeleo ya huduma za tiba ya dharura nchini, hatua iliyowezesha kuanzishwa kwa idara ya kwanza ya huduma hizo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2010.
Ameeleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa idara hiyo, wagonjwa waliokuwa wakifika hospitalini walipokelewa katika maeneo ya mapokezi na kufanyiwa vipimo vya awali kabla ya kuamuliwa kama walihitaji kulazwa au kupata huduma za wagonjwa wa nje. Hali hiyo ilionyesha umuhimu wa kuwa na mfumo maalumu wa kuwahudumia wagonjwa mahututi na majeruhi kwa haraka ili kuokoa maisha yao.
Aidha, Dkt. Kikwete amesema baada ya kuanzishwa kwa idara hiyo, alisisitiza umuhimu wa kutambua tiba ya dharura kama kada rasmi ndani ya mfumo wa afya nchini, sambamba na kuanzisha programu za mafunzo katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Amesema uwekezaji katika mafunzo ya wataalamu ulikuwa muhimu kwa kiwango sawa na uanzishwaji wa idara hizo, kwani majengo na vifaa vya kisasa pekee haviwezi kuleta mabadiliko yanayotarajiwa bila kuwapo kwa wataalamu wenye maarifa, ujuzi na dhamira ya kuokoa maisha.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana, Dkt. Kikwete amesema kuwa miaka 16 tangu kuanzishwa kwa huduma za tiba ya dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kupanua huduma hizo katika maeneo mbalimbali nchini, huku programu za mafunzo ya wataalamu zikiendelea kukua na kuimarika.
Amesisitiza kuwa maendeleo hayo ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya afya, ushirikiano wa wadau pamoja na kuweka mkazo katika kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani ili kuhakikisha wagonjwa mahututi na majeruhi wanapata huduma kwa wakati na kuongezeka kwa nafasi za kuokoa maisha.