×

Nchi za EAC Zatakiwa Kuungana Dhidi Ya Vitisho Vya Usalama Mipakani

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kukabiliana kwa pamoja na vitisho vya kiusalama vinavyovuka mipaka, ikiwemo ugaidi, makundi yenye silaha, uhalifu wa kimataifa, ukosefu wa usalama mipakani, milipuko ya magonjwa na uhalifu wa mtandaoni.

Wito huo umetolewa na Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Luteni Jenerali Jack Ngorza Okasumba, wakati akifungua Mkutano wa Wataalamu wa Ulinzi wa EAC, uliofanyika jijini Kampala, Uganda Novemba16, 2026.
Mkutano huo ulianza kwa ngazi ya Wataalamu wa Ulinzi, huku ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mkurugenzi wa Mafunzo na Elimu Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Brigedia Jenerali Benno M. Nzowa, utahitimishwa kwa mkutano wa ngazi ya Mawaziri wa Ulinzi utakaofanyika Novemba 20, 2026 jijini Kampala.

Luteni Jenerali Okasumba amesema kuwa vitisho vya kiuslama vinavyovuka mipaka haviwezi kutatuliwa na nchi moja moja, bali zinahitaji hatua za pamoja, mshikamano na ushirikiano wa karibu kati ya nchi wanachama ili kuhakikisha usalama wa kikanda unaimarika.
Ameeleza kuwa mkutano huo ni fursa muhimu kwa wataalamu wa ulinzi kujadiliana na kuoanisha misimamo kuhusu masuala ya ulinzi, pamoja na kuweka mikakati itakayoongeza ufanisi wa ushirikiano wa kiusalama katika Jumuiya.

Katika mkutano huo, wataalamu wanatarajiwa kujadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano wa ulinzi, yakiwemo pendekezo la Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja (Mutual Defence Pact), mafunzo ya pamoja ya kijeshi na ushirikiano kati ya jeshi na raia. Pia, watapitia utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita ya Baraza la Kisekta la Ushirikiano katika Masuala ya Ulinzi.

Amewapongeza nchi wanachama kwa kushiriki katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa ulinzi, huku akiipongeza Sekretarieti ya EAC kwa kuratibu mikutano hiyo ya kikanda.
Mkutano huo unafanyika kwa kuzingatia Itifaki ya EAC ya Ushirikiano katika Masuala ya Ulinzi pamoja na ratiba ya shughuli za ulinzi ya Jumuiya.

Leave a Comment