×

Miss Tanzania 2026 Kutikisa Dstv, Safari Nzima ya Washiriki Kuoneshwa Live!

Wapenzi wa mashindano ya urembo nchini Tanzania sasa kupata fursa ya kufuatilia kwa karibu safari nzima ya Miss Tanzania 2026 kupitia televisheni baada ya MultiChoice Tanzania kutangaza kuwa DStv itakuwa mshirika rasmi wa utangazaji wa mashindano hayo.

Kupitia ushirikiano huo, watazamaji wataweza kushuhudia matukio mbalimbali ya mashindano hayo kuanzia hatua za awali za kanda, maandalizi ya washiriki, kambi za mafunzo hadi Fainali Kuu itakayofanyika Desemba 19, 2026, jijini Dar es Salaam.

Vipindi hivyo vitaanza kurushwa Novemba 20, 2026 kupitia kituo cha Maisha Magic Bongo, kinachopatikana katika kifurushi cha DStv Starter kwa Shilingi 15,000 pekee. Matangazo yataendelea kila Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kwa kipindi cha wiki tano.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Tanzania, Sophie Tchatchoua, alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kampuni hiyo ya ‘Tumewasikiliza’, inayolenga kuwapatia wateja maudhui wanayoyahitaji zaidi.

Alisema wamekuwa wakipokea maoni kutoka kwa Watanzania wanaohitaji maudhui mengi zaidi ya ndani yanayoakisi maisha, vipaji na simulizi za Kitanzania, hivyo kuingizwa kwa Miss Tanzania kwenye DStv ni sehemu ya kuitikia mahitaji hayo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Miss Tanzania, Lamata Mwendamseke, alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kukuza mashindano hayo, akisisitiza kuwa Miss Tanzania si shindano la urembo pekee bali pia ni jukwaa la kujenga kujiamini, uongozi, uwajibikaji wa kijamii na uzalendo miongoni mwa wanawake vijana.

Naye Mkuu wa Maisha Magic Bongo, Evelyn Byaruhanga, alisema watazamaji watapata nafasi ya kuona mambo mengi yanayotokea nyuma ya pazia ambayo kwa kawaida hayaonekani wakati wa mashindano yanapofanyika jukwaani.

Alieleza kuwa vipindi hivyo vitaonesha maandalizi ya washiriki, changamoto wanazokutana nazo, urafiki, vikao vya ushauri na malezi, shughuli za kijamii pamoja na simulizi binafsi za washiriki katika safari yao ya kuwania taji hilo.

Aidha, watazamaji wataweza kufuatilia hatua za usaili na uteuzi wa washiriki wa kanda mbalimbali, kambi za mafunzo, shughuli za kijamii, maandalizi ya fainali na mchakato wa kuondolewa kwa washiriki kadri mashindano yanavyoendelea.

Safari hiyo itafikia kilele Desemba 19, 2026, ambapo Fainali Kuu ya Miss Tanzania 2026 itarushwa mubashara kupitia Maisha Magic Bongo kutoka jijini Dar es Salaam na kumtangaza mshindi atakayevishwa taji la mwaka huu.

Kupitia matangazo hayo, DStv inalenga kuwapa Watanzania nafasi ya kushuhudia siyo tu uzuri wa washiriki, bali pia vipaji, uwezo, changamoto na safari zao katika moja ya mashindano yenye historia na heshima kubwa nchini.

Leave a Comment