
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango, kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Uteuzi huo umetangazwa leo Novemba 17, 2026, kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Dkt. Mpango anachukua nafasi ya Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, ambaye amemaliza muda wake wa kuhudumu katika nafasi hiyo.
Katika uteuzi mwingine, Rais Samia amemteua Ezekiel Mathias Goboro kuwa Kamishna wa Uhifadhi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Aidha, Talha Mohamed Waziri ameteuliwa kuwa Balozi huku akiteuliwa pia kuwa Msaidizi wa Rais anayeshughulikia masuala ya Diplomasia.
Wengine walioteuliwa kuwa Mabalozi ni Lucas Aaron Mayanga na Dkt. Miraji Ukuti Ussi, ambao watapangiwa vituo vyao vya kazi.
Uteuzi huo ni sehemu ya mabadiliko mbalimbali ya kiutendaji katika nafasi za uongozi serikalini na taasisi za umma yaliyotangazwa na Rais Samia.
