
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Novemba 17, 2026, amewasili mkoani Tabora kwa ajili ya kushiriki harambee ya kuchangia ujenzi wa Ofisi ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Tabora.
Dkt. Mwigulu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo inayolenga kukusanya michango kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa ofisi hiyo, ambayo itakuwa muhimu katika kurahisisha shughuli za kiutawala na kuratibu shughuli mbalimbali za BAKWATA mkoani humo.

Ujio wa Waziri Mkuu unatarajiwa kuongeza hamasa kwa wadau, viongozi wa dini, waumini na wananchi kujitokeza kuchangia juhudi hizo za kuimarisha miundombinu ya taasisi hiyo ya Kiislamu.
Harambee hiyo ni sehemu ya jitihada za BAKWATA Mkoa wa Tabora katika kutafuta rasilimali zitakazowezesha kukamilisha ujenzi wa ofisi kwa ajili ya kuimarisha utendaji na huduma kwa jamii.




