×

Mahakama Yamfunga Mwalimu Aliyepata Mtoto na Mwanafunzi wa Miaka 12

Mwalimu wa zamani nchini Australia, Naomi Tekea Craig (34), amehukumiwa kifungo cha miaka minane na miezi sita jela baada ya kukiri makosa 12 ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 12 wakati vitendo hivyo vilipoanza.

Craig, aliyekuwa akifundisha muziki katika shule moja iliyopo Mandurah, kusini mwa Perth, alikutana na mvulana huyo mwaka 2023 na baadaye kujenga ukaribu na familia yake hadi kuwa rafiki wa mama wa mtoto huyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa mahakamani, mwalimu huyo alitumia ukaribu wake na familia hiyo kuendelea kuwa karibu na mvulana huyo, hata baada ya mtoto huyo kuhamia shule nyingine. Hatimaye, alipewa hata ufunguo wa nyumba ya familia hiyo.

Unyanyasaji huo ulianza mvulana akiwa na miaka 12 na kuendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kugundulika, baada ya mama wa mtoto huyo kuanza kuwa na mashaka na kufunga kamera za usalama ndani ya nyumba yao.

Picha zilizorekodiwa na kamera hizo zilikabidhiwa kwa polisi na kusaidia kufichua vitendo hivyo.

Craig alikamatwa Desemba 2025, huku akijifungua mtoto wa kike mwezi uliofuata. Vipimo vya vinasaba (DNA) vilithibitisha kuwa mvulana huyo ndiye baba wa mtoto aliyezaliwa.

Katika hukumu iliyotolewa Novemba 17, 2026, katika Mahakama ya Wilaya ya Perth, Jaji John Prior alielezea mwenendo wa mwalimu huyo kuwa ni ukiukaji mkubwa wa imani aliyokuwa amepewa na familia ya mtoto huyo.

Mahakama pia ilisikia kuwa Craig alikuwa akimnunulia mvulana huyo zawadi, kufuatilia shughuli zake kwenye mitandao ya kijamii na hata kumweleza kuwa alitamani kupata watoto zaidi naye.

Waendesha mashtaka walieleza kuwa matukio hayo yanaweza kumsababishia mvulana huyo na familia yake madhara ya kisaikolojia na kijamii ya muda mrefu.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Craig atastahili kuomba kuachiwa kwa masharti baada ya kutumikia kifungo cha miaka sita na miezi sita.

Hata hivyo, utambulisho wa mvulana huyo haujawekwa wazi kutokana na masharti ya kisheria na kulinda usalama pamoja na faragha yake.

Leave a Comment