×

Makamu wa Rais Atoa Onyo kwa Wachimbaji wa Madini, Awataka Kuzingatia Masharti ya Leseni

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amewataka wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kwa kuzingatia masharti ya leseni walizopewa, akionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa watakaokiuka taratibu hizo.

Ndejembi ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia katazo la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi, huku akizihimiza kampuni za ndani na nje kuwekeza katika viwanda vya kuchakata madini nchini hadi kufikia hatua ya bidhaa za mwisho.

Amesema uwekezaji huo utasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania, kutoa malighafi kwa viwanda vya ndani na kukuza mapato ya Taifa kupitia sekta ya madini.

Mkutano wa TMIC 2026 umewakutanisha zaidi ya wadau 1,700 kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji na namna ya kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini.

Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania, huku ajenda kuu zikihusisha uwekezaji katika madini ya dhahabu, kinywe, nikeli, shaba, madini adimu na niobiamu.

Pia, washiriki wanajadili namna ya kuongeza ushiriki wa wachimbaji wadogo na kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

 

Leave a Comment