
Klabu ya Simba SC imethibitisha kupokea malipo ya deni lake kutoka kwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids, pamoja na wasaidizi wake wawili wa zamani.
Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, kupitia ukurasa wake rasmi, akieleza kuwa deni hilo tayari limelipwa na mwajiri wa sasa wa kocha huyo.
Ahmed amesema klabu hiyo imefanikiwa kupata fedha hizo kupitia nguvu ya kisheria iliyotumika kudai haki yake, huku akieleza kuridhishwa na namna suala hilo lilivyomalizika.
“Tunapenda kuthibitisha kuwa tumepokea malipo ya deni letu kutoka kwa aliyekuwa kocha wetu Fadlu Davids yeye pamoja na wasaidizi wake wawili. Deni hilo limelipwa na mwajiri wake wa sasa,” ameandika Ahmed Ally.
Aidha, msemaji huyo ameipongeza Simba SC kwa kusimamia maslahi yake kisheria na kufanikiwa kurejesha fedha hizo.
Hatua hiyo inafunga suala la deni hilo lililokuwa likihusishwa na aliyekuwa benchi la ufundi la Wekundu wa Msimbazi, huku klabu hiyo ikionesha msimamo wake katika kudai stahiki zake.