
HARARE, ZIMBABWE– Mhubiri maarufu wa Zimbabwe, Uebert Angel, amekamatwa na polisi nchini humo kwa tuhuma za unyanyasaji wa kingono na kufanya vitendo vya ngono kinyume cha sheria.
Angel, ambaye ni mwanzilishi na kiongozi wa kanisa la kimataifa la Spirit Embassy, alikamatwa Jumapili wakati wa ibada ya kanisa jijini Harare, huku picha na video za tukio hilo zikisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.

Katika video zilizosambaa, mhubiri huyo anaonekana akiwa ndani ya gari la polisi akisindikizwa na msafara wa magari huku akizungukwa na maafisa wa polisi waliokuwa na silaha.
Polisi wa Zimbabwe wamethibitisha kukamatwa kwake, ingawa hawakutoa maelezo ya kina kuhusu mazingira ya tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa mmoja wa washirika wake, Profesa Lovemore Madhuku, Angel alikuwa bado anashikiliwa na polisi, huku muda wa kufikishwa kwake mahakamani ukiwa haujafahamika.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC), Madhuku alisema mamlaka zilikuwa bado ndani ya muda unaoruhusiwa kisheria wa kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.

Kukamatwa kwa Angel kumeibua upya mjadala kuhusu historia ya tuhuma zinazomhusu mhubiri huyo, ambaye amekuwa akitajwa katika matukio mbalimbali yenye utata.
Mwaka 2021, chombo cha habari cha ZimLIVE kilichapisha ripoti iliyodai kuwa Angel aliwahi kukabiliwa na tuhuma za utovu wa maadili ya kingono kutoka kwa wanawake kadhaa, wakiwemo angalau watano waliokuwa nchini Uingereza. Hata hivyo, mhubiri huyo alikanusha tuhuma hizo.
Aidha, mwaka 2023, Angel alitajwa katika uchunguzi wa siri uliofanywa na kituo cha televisheni cha Al Jazeera kuhusu madai ya mpango wa utakatishaji fedha kupitia biashara haramu ya dhahabu nchini Zimbabwe.

Katika uchunguzi huo, alidaiwa kupendekeza kutumia hadhi yake ya kidiplomasia kuwezesha usafirishaji wa fedha, madai ambayo pia yalihusisha jina la Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.
Angel aliteuliwa mwaka 2021 kuwa mjumbe maalumu wa rais na balozi maalumu wa Zimbabwe anayeshughulikia masuala ya Ulaya na Amerika.
Mhubiri huyo mwenye uraia wa Zimbabwe na Uingereza anafahamika kwa kuendesha huduma za kidini katika mataifa mbalimbali, yakiwemo Zimbabwe, Afrika Kusini na Uingereza.
Pia amekuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya wahubiri maarufu barani Afrika, akiwemo Shepherd Bushiri wa Malawi.
Hadi taarifa hii inaandaliwa, Angel alikuwa hajatangaza msimamo wake kuhusu kukamatwa kwake na tuhuma mpya zinazomkabili.
**Ikumbukwe kuwa kukamatwa kwa mtu hakumaanishi kuwa amepatikana na hatia; tuhuma hizo zinahitaji kuchunguzwa na kuthibitishwa kupitia taratibu za kisheria.**